Vijana wanne kati ya sita, kutoka Kenya waliotekwa nyara mwezi Desemba 2024, waliachiliwa huru kwa familia zao siku ya Jumatatu Januari 6 2025. Billy Mwangi, Peter Muteti, Bernard Kavuli, na Rony Kiplangat walikuwa wametoweka kwa wiki kadhaa, lakini wote walipatikana na kurejeshwa nyumbani salama.
Mwangi, aliyetekwa kutoka Embu, alirejea kwa familia yake katika eneo la Majengo, wakati Muteti, aliyetekwa kutoka Nairobi, alipatikana amechanganyikiwa na kutoweza kuzungumza kuhusu utekaji nyara wake. Familia yake ilithibitisha kuwa sasa anapata nafuu nyumbani. Kavuli na Kiplangat waliachwa katika mji wa Nyeri, pamoja na watu wengine waliotekwa nyara. Familia zao zilithibitisha kurudi kwao salama. Hata hivyo, jamaa wa Billy Mwangi alifichua kuwa wote walitishiwa kutozungumza kuhusu utekaji nyara wao au kuendeleza harakati zao, huku tishio la kutekwa upya likiwa limetanda juu yao.
Licha ya kurejea kwao salama, mchora vibonzo Kibet Bull bado hajulikani aliko. Familia imesikia tu kutoka kwa Kiplangat, ambaye alitoweka kabla ya Kibet. Mtu mwingine, Steve Mbisi, pia bado hajulikani aliko. Vijana hawa, pamoja na wengine kama vile Gideon Kibet, Steve Kivango, na Kelvin Muthoni, waliripotiwa kutekwa nyara kufuatia machapisho yao kwenye mitandao ya kijamii wakimkosoa Rais William Ruto na serikali yake.
Kuachiliwa kwao unaambatana na maandamano yaliyopangwa jijini Nairobi na miji mingine, ambapo waandamanaji wanataka kuachiliwa kwa wale wote ambao wametekwa nyara. Maandamano hayo yalilenga barabara kuu zikiwemo Thika Road na Mombasa Road, huku wananchi wakielezea wasiwasi wao kuhusu ongezeko la visa vya utekaji nyara chini ya utawala wa sasa.
Wimbi hili la utekaji nyara nchini Kenya limezua hasira kubwa, huku watu wengi wakihoji kuhusika kwa polisi. Wakati polisi wamekanusha kuhusika kwa vyovyote vile, mashirika ya kutetea haki za binadamu yanaendelea kutoa wito wa kufanyika uchunguzi wa kutoweka kwa vijana hao. Chama cha Wanasheria nchini Kenya (LSK) pia kimekosoa ukosefu wa hatua, na kuwataka polisi kuchunguza na kuwashtaki waliohusika au kujiuzulu.
Katika kukabiliana na mvutano huo unaoongezeka, Rais William Ruto hivi majuzi aliahidi kukomesha utekaji nyara nchini. Aliapa kuwa vijana wataruhusiwa kuishi kwa amani na kwamba serikali itachukua hatua kuhakikisha usalama wao. Hata hivyo, hali bado si shwari nchini, huku watu wengi wakiwemo wanaharakati maarufu na wakosoaji wa serikali wakiendelea kutoweka.