Search
Close this search box.
East Africa
Viongozi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki katika mkutano wa pamoja katika Ikulu ya Nairobi, Kenya. Juni 20, 2022

Viongozi wa Afrika Mashariki walikubaliana Jumatatu kutuma kikosi cha kikanda kujaribu kumaliza mapigano mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, na kutoa wito wa kusitishwa mara moja kwa mapigano.

Hatua hiyo ilitangazwa na ofisi ya rais wa Kenya baada ya nchi wanachama saba wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kufanya mazungumzo mjini Nairobi kuhusu kushamiri kwa ghasia katika eneo hilo lenye hali tete.

“Wakuu wa nchi waliagiza kwamba jeshi la kikanda linapaswa, kwa ushirikiano na jeshi na vikosi vya utawala vya DRC, kuleta utulivu na kulinda amani nchini DRC,” ofisi ya Rais Uhuru Kenyatta ilisema katika taarifa.

“Wakuu wa nchi waliagiza kwamba usitishaji vita wa mara moja utekelezwe na usitishaji wa mapigano uanze mara moja.”

DRC yenye utajiri mkubwa wa madini inajitahidi kudhibiti makumi ya makundi yenye silaha mashariki mwa nchi, ambayo mengi ni urithi wa vita viwili vya kikanda robo karne iliyopita.

Kuzuka kwa mapigano makali hivi karibuni mashariki mwa nchi kumefufua chuki za miongo kadhaa kati ya Kinshasa na Kigali, huku DRC ikiilaumu nchi jirani ya Rwanda kwa kuzuka upya kwa wanamgambo wa M23.

Rwanda imekanusha mara kwa mara kuwaunga mkono waasi, huku nchi zote mbili zikilaumiana kwa kufanya mashambulizi ya mipakani.

Taarifa ya Kenya haikusema kama wanajeshi wa Rwanda watahusika katika jeshi la kikanda — lakini serikali mjini Kinshasa ilisisitiza kuwa haitakubali kuwepo kwao.

“Kikiwa chini ya uongozi wa kijeshi wa Kenya, kikosi hiki kinafaa kufanya kazi katika wiki zijazo na kisijumuishe ndani yake wahusika wa jeshi la Rwanda,” ofisi ya rais wa DRC ilisema kwenye Twitter.

Rais wa DRC Felix Tshisekedi na Paul Kagame wa Rwanda walikuwa kwenye mkutano huo ulioandaliwa na Kenyatta, pamoja na viongozi wa Burundi, Sudan Kusini na Uganda, na balozi wa Tanzania mjini Nairobi.

Kagame alihudhuria ingawa Rwanda inakaribisha makumi ya viongozi kutoka kote ulimwenguni katika Mkutano wa Wakuu wa Serikali wa Jumuiya ya Madola (CHOGM) baadaye wiki hii.

Mkuu wa Tume ya Umoja wa Afrika Moussa Faki Mahamat amekaribisha matokeo ya mazungumzo hayo katika taarifa iliyochapishwa kwenye Twitter.

“Naomba kutekelezwa mara moja kwa maamuzi yao ili kurejesha amani Mashariki mwa DRC,” aliongeza.

Wanamgambo wa Kitutsi wa Kongo, M23 walipata umaarufu duniani mwaka 2012 walipouteka mji mkuu wa mashariki mwa DRC wa Goma.

Ililazimishwa kuondoka muda mfupi baadaye katika mashambulizi ya pamoja ya wanajeshi wa Umoja wa Mataifa na jeshi la Kongo.

Lakini hivi karibuni wanamgambo wamerejea tena, wakipambana na wanajeshi wa Kongo katika ghasia ambazo zimezusha hali ya wasiwasi katika eneo la Afrika ya kati na kuwalazimu maelfu ya watu kukimbilia nchi jirani ya Uganda.

“Matatizo yanayoathiri eneo kama vile mgogoro wa Kongo yanahitaji mbinu ya pamoja kutoka kwa wanachama wote wa kikanda wa Jumuiya ya Afrika Mashariki,” Rais wa Uganda Yoweri Museveni alisema kwenye Twitter wakati mkutano ukiendelea.

Baada ya waasi wa M23 kuuteka mji wa mpaka wa Bunagana wiki moja iliyopita, Kenyatta alitoa wito wa kutumwa kwa kikosi cha EAC kurejesha amani, na wakuu wa kijeshi kutoka nchi saba wanachama wa umoja huo walikutana Jumapili.

Wakati huo huo, M23 ilisema inafungua tena kituo cha mpaka cha Bunagana, kituo chenye shughuli nyingi za biashara na usafirishaji wa bidhaa ambacho hakiko mbali na mstari wa mbele.

Tshisekedi ameishutumu Rwanda kwa kutaka ‘kuchukua ardhi yetu,’ ambayo ina madini mengi kama vile dhahabu, coltan na cobalti ‘kwa ajili ya kujinufaisha.”

Ametoa wito kwa jumuiya ya kimataifa, na hasa Uingereza, ‘kuishinikiza Rwanda kuondoa wanajeshi wake,’ akibainisha makubaliano yenye utata ya London ya kutuma waomba hifadhi mjini Kigali.

“Kwa kuzingatia makubaliano ya hivi majuzi ya Uingereza na Rwanda kuhusu uhamiaji, tunatumai kuwa Waziri Mkuu Boris Johnson ataweza kuongeza ushawishi wake,” Tshisekedi alisema.

Uhusiano kati ya Kinshasa na Kigali umekuwa mbaya tangu kuwasili nchini DRC kwa Wahutu wa Rwanda wanaotuhumiwa kuwaua Watutsi wakati wa mauaji ya halaiki ya Rwanda mwaka 1994.

Comments are closed