Waasi wa kundi la M23 siku ya Jumapili walitangaza kuondoka katika vijiji vilivyotekwa mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo kufuatia mapigano na wanajeshi wa serikali katika eneo la Rutshuru.
Mapigano kati ya waasi na wanajeshi yalipamba moto Jumatano baada ya siku kadhaa za utulivu na waasi wa M23 walichukua udhibiti wa karibu vijiji kumi na mbili katika eneo la Rutshuru katika jimbo la Kivu Kaskazini, duru za ndani zilisema.
Kundi la M23 lilichukua “uamuzi wa kujiondoa, kwa mara nyingine tena, kutoka kwa ngome zao … ili kuruhusu matakwa yao kushughulikiwa kwa njia ya mazungumzo ya wazi na yenye manufaa na serikali” ya DR Congo, kundi hilo lilisema.
M23 “hawakuwa na nia ya kukamata maeneo na kuyadhibiti, motisha wetu pekee ni utatuzi wa amani wa mgogoro,” iliongeza katika taarifa.
Lakini haikuthibitishwa kufikia adhuhuri Jumapili ikiwa wamejiondoa kutoka vijiji walivokuwa wameteka.
M23 pia ilisema inakusudia ‘kuwakabidhi’ (wanajeshi) wote kutoka kwa jeshi la kitaifa waliokamatwa kwenye mstari wa mbele kwa Kamati ya Kimataifa ya Msalaba Mwekundu.
Kundi la M23 lilianzishwa miongoni mwa wanachama wa zamani wa wanamgambo wa Kitutsi wa Congo ambao wakati fulani waliungwa mkono na Rwanda na Uganda.
Waasi hao walikuwa wamejumuishwa katika jeshi la Congo chini ya mkataba wa amani uliotiwa saini Machi 23, 2009. Mnamo mwaka wa 2012, waliasi, wakisema mpango huo haujafuatiliwa na wakataja kundi lao kuwa March 23 (M23) Movement.
Wakiwa miongoni mwa makundi mengi yenye silaha ambayo yanazunguka mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, M23 waliuteka kwa muda mji wa Goma kabla ya kushindwa na kulazimishwa kuondoka nchini humo.
Baada ya kushindwa, M23 hatimaye ilitia saini makubaliano na Kinshasa ambayo yalijumuisha masharti ya wapiganaji wake kujumuika tena na kiraia.
Lakini kundi hilo limeishutumu tena serikali kwa kughairi mpango huo na kuanza tena mapigano mwaka jana. Shambulio lao la hivi punde lilianza mwishoni mwa Machi.