Wachimba migodi nchini Angola wamechimba almasi isiyo ya kawaida ya karati 170 ya waridi ambayo inaaminika kuwa kubwa zaidi kupatikana katika miaka 300, kulingana na kampuni ya uchimbaji madini ya Australia.
Almasi hiyo adimu imepewa jina âLulo Roseâ iligunduliwa katika mgodi wa Lulo nchini Angola na Kampuni ya Lucapa Diamond.
Kampuni ya Almasi ya Lucapa ilisema katika taarifa yake kwa wawekezaji kwamba ni miongoni mwa almasi kubwa zaidi ya waridi kuwahi kupatikana katika historia.
Upatikanaji wa almasi ya aina ya IIa sasa umepokelewa na serikali ya Angola, ambayo pia ni mshirika katika mgodi huo.
Almasi ya aina ya IIa ni moja wapo ya aina adimu na safi zaidi ya madini asili.
âAlmasi hii ya kuvutia ya waridi iliyopatikana huko Lulo inaendelea kuonyesha Angola kama moja ya mataifa yenye utajiri wa madini.â Waziri wa Rasilimali Madini wa Angola Diamantino Azevedo alisema.
Ripoti zinasema almasi hiyo itauzwa kwa mnada wa kimataifa.
Lakini kabla ya hapo, inabidi ikatwe na kungâarishwa ili kudhihirisha thamani yake halisi, katika mchakato ambao unaweza kupunguza uzito wa almasi hiyo.
Hapo awali, almasi za waridi sawa ziliuzwa kwa bei iliyovunja rekodi katika soko la kimataifa.
Kwa mfano, Pink Star ya karati 59.6 iliuzwa katika mnada wa Hong Kong mwaka wa 2017 kwa dola za Marekani milioni 71.2.
Hadi leo, inasalia kuwa almasi ghali zaidi kuwahi kuuzwa.
Kufuatia ugunduzi huo, waziri wa rasilimali za madini wa Angola Diamantino Azevedo alisema kuwa Angola ni mdau muhimu wa kimataifa katika uchimbaji wa almasi.
âInaonyesha wazi faida ya kujitolea na uwekezaji katika sekta yetu inayokua ya uchimbaji madini ya almasi,â waziri aliongeza.