Wadau wa haki Tanzania Wataka adhabu ya kifo iondolewe

Wadau wa haki jinai nchini Tanzania wameiomba serikali kuangalia uwezekano wa kuweka adhabu mbadala kwa kosa la mauaji badala ya kunyongwa hadi kufa kwa kuwa haijawahi kutekelezwa tangu serikali ya awamu ya tatu ya hayati rias Benjamin William Mkapa huku wafungwa wengi wakikaa magerezani wakizidi kuteseka kisaikolojia.

Akizungumza na wanahabari, wakatiki wa maadhimisho ya Siku ya Kupinga Adhabu ya Kifo Duniani yenye kaulimbuiu ‘Adhabu ya Kifo Hailindi Mtu Yeyote: Iondolewe Sasa’,  shirika hilo lilisema wafungwa hao nchini Tanzania  ni mzigo kwa serikali kutokana na kutunzwa kwa fedha za Watanzania.

 

Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Dk. Anna Henga, alisema lengo la adhabu ni kurekebisha tabia ili mtu awe mfano kwa wengine lakini wengi wako gerezani kwa muda mrefu na hawajui hatima yao.

“Adhabu ya kifo haifanyi kazi yoyote kwa kuwa wanalishwa kwa gharama za serikali, hivyo ni mzigo kwa taifa, Adhabu hii haijawahi kutekelezwa mwaka 1994. Ni  miaka 30 sasa. Kama  imeshindikana kutekelezwa ni muhimu kukawa na mbadala,” alisema.

Pia alisema hakuna ushahidi kwamba adhabu hiyo imepunguza uhalifu bali kumekuwa na makosa mengi na kwamba hivi karibuni nchini  Iran, kuna adhabu ya kifo na hata mwizi wa simu anapata adhabu hiyo na kwamba wamenyonga zaidi ya 200 lakini bado matukio yapo.

Dk. Henga alisema wako waliohukumiwa kifo kimakosa na baada ya muda wanaachiwa baada ya kukata rufani huku wengine hawajui taratibu ili wapate msaada kisheria na kwamba mtu anaponyongwa hakuna namna yoyote inawezekana kumrejesha.

“Tanzania ni nchi ya demokrasia lakini kutokana na mizizi ya kikoloni ndiyo maana sheria hiyo imeendelea kuwapo. Kuna mikataba mingi tumeridhia ukiwamo Mkataba wa Haki za Binadamu na Kiraia ambao unatambua haki za kuiishi,” alisema.

Kuhusu sababu za mauaji, wachangiaji hao walisema wengi walioko gerezani ni kwa sababu ya kulipiza kisasi, wivu wa kimapenzi, imani za kishirikiana kutaka kupata utajiri na msongo wa mawazo.