Nchini Burkina Faso, mamia ya wafanyakazi wanasema wamefurahishwa na kupinduliwa kwa rais wa nchi hiyo Roch Kabore. Wafanykazi wanasema aliwaacha wafe njaa, na sasa wanatarajia mustakabali mwema chini ya wanajeshi waliompindua.
Niamba Azara, mwanamke anayefya kazi ya kufagia barabara, alikuwa miongoni mwa watu wengi nje ya kituo cha wafanyikazi cha Ouagadougou siku ya Alhamisi ambao walisema hawajapokea mishahara kwa mwaka mmoja.
“Tumekuwa ombaomba,” alisema.
Mapinduzi haya ni “habari njema kwetu. Nchi iko katika hali mbaya.
Karibu naye, wengine pia walifurahi jeshi liliponyakua mamlaka kutoka kwa kiongozi wa zamani Roch Marc Christian Kabore wiki hii.
“Rais wa zamani hakutaka wafanyikazi wale.” alidai Assami Ouedraogo, mtunza bustani katika mji mkuu.
“Tunafurahi walimuondoa.”
Burkina Faso imezama katika mzozo wa usalama tangu 2015, na karibu kila siku mashambulizi ya wanajihadi yanaathiri maeneo mengi ya nchi hiyo.
Watu wengi katika nchi hiyo ya Afrika Magharibi katika miaka ya hivi karibuni wamezidi kufadhaishwa na kushindwa kwa rais huyo wa zamani kuzima uasi huo.
Lakini malalamishi ya kijamii pia yalichochea machafuko yaliyofikia kilele siku ya Jumatatu baada ya kuondolewa kwa Kabore, mwanabenki aliyechaguliwa mwaka wa 2015.
Katika ofisi za ajira, wafanyikazi walisema hawajapokea malipo yoyote tangu Februari 2021 kutoka kwa meya wa Ouagadougou Armand Beouinde, ambaye anajulikana kuwa mwandani wa rais aliyepinduliwa.
Chanzo cha habari katika ofisi ya meya hata hivyo kilisema wanaodai mishahara ni vibarua wanaofanya kazi mchana kutwa ambao hawakuwahi kuajiriwa kwa mikataba ya kudumu na ilibidi wabadilishwe baada ya mgomo.
Ismael Ouedraogo, mwanamume mwenye umri wa miaka sabini, aliugua baada ya miaka 16 ya kufanya kazi ya kukusanya taka mjini Ouagadougou.
“Tulitendewa kama watumwa, wafungwa wanaofanya kazi bila kulipwa,” alisema.
“Sijawahi kuajiri rasmi, sijawahi kupata pensheni au likizo, na sasa sina hata mshahara. Pensheni yetu ni kifo.”
“Wanataka nini? Wanataka tuwe majambazi? Wanajihadi?”
Asilimia 40 ya wakazi wa Burkinabe wanaishi maisha ya uchochole kulingana na Benki ya Dunia.
Burkina Faso ipo katika nafasi ya 182 kati ya nchi 189 kwenye faharasa ya maendeleo ya binadamu ya Mpango wa Maendeleo wa Umoja wa Mataifa.
Maafisa wa vyama vya wafanyakazi wanasema kima cha chini cha kila mwezi cha mshahara kimekwama kuwa sawa na dola 50 tangu 2008.
Maandamano hayo “vitendo vya wafanyakazi hao vilichochea kufadhaika na hasira miongoni mwa watu wa Ouagadougou,” mwakilishi mmoja wa chama hicho, Banogo Noufe alisema.
“Kwa mapinduzi haya” askari walikamilisha kazi.”
Abdoulaye Tao, mhariri mkuu wa gazeti la kila wiki la Economiste du Faso, anasema kuna pengo kati ya matajiri na maskini nchini humo, “na wameshindwa kupunguza tofauti hiyo.”
“Maisha ya kifahari ya viongozi wa umma, malalamiko ya ufisadi kati ya wakuu wa nchi yaliharibu hali zaidi… wananchi hawajaona mamlaka zikifanya wakiweka jitihada zozote,” alisema.