Tume ya uchaguzi ya Libya ilisema Jumanne kuwa wagombea 98, wakiwemo wanawake wawili, wamejiandikisha kuwania katika uchaguzi wa rais unaotarajiwa kufanyika Disemba.
“Jukwaa la usajili wa wagombea limepokea karatasi za wagombea 98 ambao walitimiza masharti,” mkuu wa tume ya uchaguzi, Imad al-Sayeh, aliuambia mkutano wa waandishi wa habari mjini Tripoli.
Miongoni mwa watu wenye matumaini makubwa ni Seif al-Islam Kadhafi, mwanawe dikteta aliyeuawa Moamer Kadhafi, na Khalifa Haftar, kiongozi wa wanaojiita Jeshi la Taifa la Libya linalodhibiti eneo la mashariki na maeneo ya kusini mwa nchi hiyo.
Wengine wanaowania ni waziri wa zamani wa mambo ya ndani Fathi Bashagha na Waziri Mkuu Abdulhamid Dbeibah wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa iliyosimamiwa na Umoja wa Mataifa.
Ni wanawake wawili tu wamejitokeza kama wagombea: Laila Ben Khalifa, mwenye umri wa miaka 46, rais na mwanzilishi wa chama cha National Movement, na Hunayda al-Mahdi, mtafiti katika sayansi ya jamii.
Uchaguzi unakuja wakati Umoja wa Mataifa unataka kumaliza muongo mmoja wa ghasia ambazo zimetikisa taifa hilo lenye utajiri mkubwa wa mafuta tangu ghasia zilizoungwa mkono na NATO kumwangusha na kumuua Kadhafi mwaka wa 2011.
Orodha ya mwisho ya wagombeaji itachapishwa ndani ya siku 12, mara tu uthibitishaji na rufaa zitakapokamilika, alisema Sayeh, siku moja baada ya tarehe ya mwisho ya kuwasilisha maombi.
Tume hiyo “itawasilisha karatasi kwa mwendesha mashtaka mkuu, idara ya pasipoti na utaifa na kwa Mkuu wa Ujasusi” ili kuhakikisha wagombeaji wanazingatia sheria ya uchaguzi.
Uandikishaji wa kura ya kwanza ya moja kwa moja ya urais nchini Libya tarehe 24 Disemba ulifanyika katika ofisi tatu za tume mjini Tripoli upande wa magharibi, Benghazi mashariki na Sebha kusini.
Zaidi ya watu milioni 2.8 kati ya watu milioni saba wa Libya wamejiandikisha kupiga kura. Mkuu wa tume ya uchaguzi alisema hadi sasa “zaidi ya wapiga kura milioni 1.7 wamepokea kadi zao (za kupiga kura).”