Takriban wahamiaji 23 ambao walikufa mwezi uliopita katika jaribio la kuingia katika eneo la Uhispania la Melilla kutoka Morocco huenda “walikosa hewa,’ shirika la kutetea haki za binadamu la CNDH linaloungwa mkono na serikali ya Morocco lilisema Jumatano.
Idadi ya vifo baada ya watu wapatao 2,000, wengi kutoka Sudan, kuvamia mpaka tarehe 24 Juni ilikuwa mbaya zaidi kuwahi kutokea katika miaka ya majaribio ya wahamiaji kuvuka maeneo ya Ceuta na Melilla ya Uhispania, ambayo yana mipaka miwili pekee ya Umoja wa Ulaya na Afrika.
Adil El-Sehimi, daktari ambaye aliichunguza miili hiyo alisema wahamiaji hao walikuwa na uwezekano mkubwa wa kufa kwa “kukosa hewa,’ wakati nguvu au kitu kinamzuia mtu kupumua.
Mkuu wa CNDH Amina Bouayach alisema wahamiaji 23 walifariki katika tukio hilo, na kuthibitisha idadi rasmi ya waliouawa.
Hakuna hata mmoja wa waliofariki ambaye amezikwa na uchunguzi wa maiti ulikuwa ukisubiriwa, Bouayach aliuambia mkutano wa waandishi wa habari mjini Rabat alipokuwa akiwasilisha matokeo ya awali ya uchunguzi wa CNDH.
Kundi la kutetea haki la Uhispania la Caminando Fronteras linasema takriban watu 37 walipoteza maisha.
Siku tano baada ya tukio hilo, Human Rights Watch (HRW) ilitaja ‘ripoti kwamba mamlaka nchini Morocco huenda ikafanya maziko ya pamoja’ baada ya ushahidi wa picha wa makaburi yaliyochimbwa hivi karibuni katika eneo la karibu la Nador kuchipuka.
CNDH ilisema idadi kubwa ya wahamiaji, ‘waliojihami kwa fimbo na mawe… walijigawanya katika makundi mawili: la kwanza lilivamia nguzo ya mpaka iliyofungwa tangu 2018 na la pili lilipanda kuta za karibu zilizowekwa juu kwa waya.”
Ilisema kwamba wafu walikuwa wamepondwa karibu na sehemu ya kituo cha mpaka,lenye mapango ambayo huruhusu mtu mmoja kupita kwa wakati mmoja.
“Idadi kubwa ya wahamiaji walijikuta wakisongamana katika eneo hili nyembamba, na kusababisha msongamano ambao ulisababisha wahamiaji kukosa hewa,”ilisema.
Umoja wa Mataifa, Umoja wa Afrika na mashirika huru ya kutetea haki za binadamu yamelaani matumizi ya nguvu kupita kiasi yanayofanywa na maafisa wa usalama wa Morocco na Uhispania.
HRW ilisema video ilionyesha maafisa wa usalama wa Morocco akiwapiga wanaume waliojeruhiwa chini na afisa mwingine akitupa mwili uliolegea kwenye rundo la watu.
CNDH ilitetea hatua za vikosi vya Morocco, ikisema kesi kama hizo ni za kipekee na kutaja hatari inayoletwa na idadi kubwa ya wahamiaji kubeba fimbo na mawe.