Wakenya lazima watii sheria! Rais Ruto asema baada ya maandamano

Rais William Ruto akizungumza katika ziara ya kidiplomasia nchini Ujerumani

Rais William Ruto mnamo Jumanne alisema ni lazima Wakenya wote watii sheria siku moja baada ya maandamano dhidi ya serikali kuwa ghasia huku polisi wakifyatua vitoa machozi na waporaji wakiendelea na fujo.

Muungano wa Afrika ulitoa wito wa kuwepo kwa mazungumzo ya utulivu na kisiasa baada ya maandamano yaliyoitishwa na kiongozi wa upinzani Raila Odinga kutikisa Nairobi na jiji la Kisumu.

Kiongozi huyo mkongwe wa upinzani ameitisha maandamano ya mara kwa mara kila Jumatatu na Alhamisi, akimshutumu Ruto kwa kuiba uchaguzi wa mwaka jana na kushindwa kudhibiti kupanda kwa gharama ya maisha.

Ruto ambaye yuko katika ziara ya kidiplomasia nchini Ujerumani, alisema hali ya kutoadhibiwa haitavumiliwa na Wakenya wote lazima watii sheria.

“Hilo ndilo linalotufanya kuwa sawa. Hakuna anayefaa kukanyaga haki za wengine,” Ruto alisema kwenye taarifa, akiongeza kuwa atahakikisha haki ya kuishi, mali na biashara inalindwa.

“Tumewapa polisi uhuru wa kiutendaji na kifedha kwa makusudi kufanya kazi, ni jukumu lao kuhakikisha kila mtu anafuata sheria,” alisema.

Siku ya Jumatatu, polisi walirusha vitoa machozi Nairobi na Kisumu kutawanya umati wa watu, wakilenga magari yaliyokuwa yamebeba wanahabari katika mji mkuu.