Baada ya muungano wa Azimio la umoja kutangaza kuwa watakuwa wanawasilisha kesi mahakamani kupinga matokeo ya uchaguzi wa urais jinsi ilivyotangazwa na tume ya uchaguzi nchini Kenya IEBC, sasa wakenya wanaangazia mahakama ya upeo.
Ijapokuwa viongozi wa Azimio la Umoja walisema watatumia njia za kisheria kubatilisha ushindi wa William Ruto, bado hawajawasilisha kesi katika mahakama ya upeo.
“Sitaki kuzungumzia kwa mapana mikakati yetu kuendelea mbele ila tutatumia njia za kikatiba na kisheria kupinga matokeo yaliotangazwa na Chebukati,” alisema Odinga wakati akipinga matokeo hayo.
Iwapo kesi itawasilishwa, itaskizwa na kuamuliwa na jopo la majaji saba wakiongozwa na jaji mkuu Martha Koome.
Majaji wengine wa mahakama ya upeo ni naibu jaji mkuu Philomena Mwilu, Jaji Mohamed Ibrahim, Smokin Wanjala, Njoki Ndumg’u, Isaac Lenaola na Willian Ouko.
Kwa mujibu wa katiba ya Kenya, mahakama ya upeo inafaa kuskiza na kuamua kesi hiyo ndani ya siku 14 baada ya kesi kuwasilishwa mahakamani.
Mtu yeyote anayetaka kupinga matokeo ya uchaguzi wa urais ako na siku saba baada ya matokeo hayo kutangazwa kuwasilisha kesi mahakamani, hii ina maana kuwa Muungano wa Azimio au mkenya yeyote anayetaka kupinga kuchaguliwa kwa rais mteule William Ruto anafaa kufanya hivyo kufikia jumatatu tarehe 22 mwezi huu wa agosti.
Hata hivyo iwapo kesi haitawasilishwa makamani, rais mteule Ruto na naibu rais mteule Rigathi Gachagua wataapishwa agosti tarehe 30 ikiwa jumanne ya kwanza inayofuata siku 14 baada ya matokeo kutangazwa.
Na iwapo kesi iliyowasilishwa itaidhinisha kuchaguliwa kwao basi wawili hao wataapishwa jumanne ya kwanza inayofuata siku saba baada ya mahakama ya upeo kutoa uamuzi wake.
Raila Odinga ambaye alipoteza azma ya kuwa rais wa Kenya kwa mara ya tano alipinga matokeo kwa misingi kuwa zoezi la uchaguzi ulifanywa pasi na kuzingatia uwazi.
Muungano wake wa Azimio ukitarajia kutumia mgawanyiko kati ya makamishna wa IEBC baada ya baadhi yao kupinga matokeo yaliotangazwa na mwenyekiti Wafula Chebukati kama ushindi wao kwenye kesi hiyo.
Naibu wa mwenyekiti Juliana Cherera na makamishna Irene Masit, Francis Wanderi na Justus Nyang’aya walidai kuwa menyekiti wa IEBC Wafula Chebukati alitangaza matokeo ambayo kwa pamoja yalikuwa asilimia 100.01, madai ambayo baadaye walijulikana kuwa sivyo.
Hapo jana Chebukati alitoa taarifa kwa vyombo vya habari akisema wanne hao walijitenga na matokeo hayo baada yake kudinda kusawazisha matokeo ya urais ili kulazimu marudio ya uchaguzi jinsi walivyotaka.
Matokeo ya kila uchaguzi umekuwa ukipingwa nchini Kenya tangu mwaka wa 2002 na Odinga anashikilia kuwa alinyimwa ushindi wake katika chaguzi za mwaka wa 2007, 2013 na 2017.