Hospitali kuu ya umma nchini Kenya inasema kumekuwa na ongezeko la idadi ya watu wanajitolea kuuza figo zao.
Hospitali ya Kitaifa ya Kenyatta (KNH) imekubali wazi kuwa kumekuwa na maombi mengi kutoka kwa Wakenya wanaotaka kuuza viungo vyao kwa hospitali hiyo kubwa zaidi ya rufaa nchini.
Kulingana na wasimamizi wa hospitali hiyo, wamekuwa wakipokea maswali mengi kutoka kwa watu wanaotaka kufanya biashara ya figo zao.
KNH hata hivyo imefafanua kuwa uuzaji wa figo, na viungo vingine ni haramu nchini humo na mtu anaweza tu kujitolea kwa hiari yake.
âTafadhali kumbuka kuwa uuzaji wa viungo ni marufuku kabisa na ni haramu, Unaweza tu kujitolea kwa hiari yako,â ilisema hospitali hiyo.
Benki ya Dunia mapema mwezi huu ilionya kuwa Afrika Mashariki ni miongoni mwa maeneo yanayokabiliwa na mdororo mkubwa wa uchumi kwa sababu ya vita vya Urusi nchini Ukraine na janga la UVIKO 19.
Wakenya wameathirika na kupanda kwa gharama za bidhaa za kimsingi kama vile chakula na mafuta, mzozo uliochochewa na vita vya Ukraine, huku maeneo kadhaa ya nchi pia yakikumbwa na ukame mkali.
Rais Uhuru Kenyatta, katika sherehe za Siku ya Wafanyakazi mnamo Mei 1, alitangaza nyongeza ya asilimia 12 ya mshahara wa chini ili kuwasaidia wafanyikazi wanaokabiliwa na gharama ya juu ya maisha ingawa agizo hilo limesalia kuwa ahadi ambayo bado haijatekelezwa.
Kulingana na takwimu rasmi, mfumuko wa bei wa Kenya mwezi Aprili ulipanda hadi kiwango cha juu cha miezi saba hasa kutokana na kupanda kwa bei ya mafuta na vyakula.
Wakati wa hotuba yake mnamo Mei 1, Kenyatta alisema gharama kubwa ya maisha ilitokana na âmambo ambayo yamekwenda nje ya uwezo wangu kama janga la coronavirus na mzozo wa Urusi na Ukraine.â
Ingawa ni haramu katika nchi nyingi duniani kote, biashara ya figo ni miongoni mwa biashara za siri zenye faida kubwa, huku madalali wakitumia mitandao ya kijamii kutafuta wafadhili.
Kulingana na Shirika la Afya Duniani (WHO), Asia Kusini ndio kitovu cha uuzaji wa figo ulimwenguni, huku India ikiwa miongoni mwa wauzaji wa juu wa figo.
Inakadiriwa kuwa zaidi ya Wahindi 2,000 huuza figo zao kila mwaka, nyingi zikiwa ni za wageni.
Kuongezeka kwa magonjwa ya figo, kisukari na shinikizo la damu kunasababisha hitaji la kimataifa la figo, ambalo linapita usambazaji wa kiungo hicho muhimu kulingana na sheria.
Kutokana na hali hiyo, India, Nepal, Bangladesh, Pakistan, Sri Lanka na Iran zimekuwa soko kubwa zaidi la uuzaji haramu wa viungo.
Plasma ya damu, manii na nywele ni baadhi ya viungo vingine vinavyoingiza pesa nyingi.