Wakili Boniface Mwabukusi ashinda rufaa, kuwania urais TLS

Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam imetoa hukumu ya kesi iliyokuwa imefunguliwa na Wakili wa kujitegemea Boniface Mwabukusi dhidi ya Chama cha Mawakili Tanganyika (TLS) ambapo Wakili Mwabukusi alikuwa akipinga uamuzi wa kamati ya rufani kumuengua kugombea urais wa chama hicho katika uchaguzi unaotarajiwa kufanyika mapema mwezi Agosti mwaka huu.

TLS ilikuwa imemwengua kugombea nafasi hiyo tarehe 5 Julaimwaka Huu

Katika hukumu iliyotolewa leo, Ijumaa Julai 26,2024 na Jaji Phillip Butamo, mahakama imeeleza kuwa imeridhika na hoja zilizotolewa na upande wa Boniface Mwabukusi ambapo ni  sasa rasmi imetengua maamuzi ya kamati ya rufani ya TLS.

Kufuatia uamuzi wa mahakama kuu, Wakili Mwabukusi amerejeshwa kugombea nafasi ya urais wa TLS.

Mwabukusi alikuwa mmoja wa wanachama walioomba na kupitishwa na Kamati ya Uchaguzi kugombea nafasi ya urais wa TLS, lakini akapingwa kwenye kamati ya maadili ambayo ilimwengua.

Uchaguzi wa TLS unatarajiwa kufanyika Agosti 1-3, 2024 jijini Dodoma.