Wakimbizi milioni moja wamekimbia Ukraine katika wiki moja tangu uvamizi wa Urusi, Umoja wa Mataifa ulisema Alhamisi, ukionya kwamba mashambulio hayo yasipoisha mara moja, kuna uwezekano wa mamilioni wengine kukimbia.
Viongozi wa Umoja wa Mataifa pia waliomba kila anayetoroka atendewe sawa, huku wakitoa tahadhari kutokana na ripoti za raia wa Afrika na Asia wanaokabiliwa na ubaguzi kwenye mpaka.
“Katika muda wa siku saba tu tumeshuhudia kuhama kwa wakimbizi milioni moja kutoka Ukraine hadi nchi jirani,”mkuu wa Umoja wa Mataifa wa wakimbizi Filippo Grandi alitweet.
“Iwapo mzozo hautakomeshwa mamilioni zaidi wanaweza kulazimika kuikimbia Ukraine,” alionya.
Kulingana na data kutoka kwa shirika la Grandi la UNHCR, watu 1,045,459 sasa wameikimbia Ukraine tangu Rais wa Urusi Vladimir Putin aanzishe uvamizi Februari 24.
Grandi alisema kuwa katika takriban miaka 40 wakifanya kazi kushughulikia wakimbizi,”ni mara chache sana nimeona uhamisho wa haraka kama huo.”
Zaidi ya nusu ya wale ambao wamekimbia Ukraine — karibu watu 548,000 – wamevuka magharibi na kuingia Poland, UNHCR ilisema.
Walinzi wa mpaka wa Poland walisema zaidi ya watu 600,000 kwa jumla wamevuka mpaka – wengi watakuwa wamehamia maeneo mengine Ulaya – na watu 56,400 wakivuka Alhamisi, kufikia saa 1400 GMT.
Watoto nusu milioni
Hungary, Moldova, Slovakia na Romania pia wamepokea makumi ya maelfu ya wakimbizi.
Watu wengi pia wamefurushwa ndani ya Ukraine.
Grandi alipongeza mwitikio ‘wa ajabu’ wa serikali na jumuiya za wenyeji katika nchi jirani ambazo zimepokea mamilioni ya wakimbizi.
Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF limesema kuwa nusu ya walioondoka Ukraine ni vijana.
“Watoto nusu milioni tayari wameikimbia Ukraine hadi nchi jirani, huku idadi ya wakimbizi ikiendelea kuongezeka,” ilisema taarifa yake.
UNICEF ilisema inaweka ‘maeneo salama’ kwa watoto na akina mama kupata huduma kwenye njia za usafiri.
Mkuu wa misaada wa Umoja wa Mataifa Martin Griffiths alisema idadi ya wakimbizi ‘taendelea kuongezeka haraka sana, kwa saa’.
Huku majeshi ya Urusi yakikaribia miji mikubwa, watu wengi wanaendelea kuhama kutoka kubaki hadi kuondoka na :tutaona watu wengi zaidi wakiyahama makazi yao.” aliiambia AFP.
Alionya wahusika katika mzozo kwamba wana jukumu la kulinda raia ndani ya Ukraine na “wale wanaohama wahame salama, ikiwa wanataka”.
Wasiwasi wa ubaguzi
Mkuu wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa Michelle Bachelet alisema wakimbizi hao milioni mara nyingi walitumia siku nyingi kusafiri kwa baiskeli au kwa miguu kwenye baridi kali.
Lakini aliibua wasiwasi juu ya wakimbizi wasiokuwa Waukreni ambao, baada ya kufika mipakani, walikabiliwa na ubaguzi.
“Ninapongeza makaribisho ambayo raia wa Ukraine wanaoondoka nchini wamepokea. Mapokezi haya lazima yatolewe kwa wale wote wanaokimbia migogoro, bila kujali uraia wao, kabila, uhamiaji au hali nyingine,” aliambia Baraza la Haki za Kibinadamu la Umoja wa Mataifa.
“Kumekuwa na ripoti za kutatanisha za ubaguzi dhidi ya raia wa Afrika na Asia wakati wakitoroka mashambulizi.
Kiongozi wa Shirika la Kimataifa la Uhamiaji Antonio Vitorino pia alielezea wasiwasi wake, akisema wafanyakazi wa kigeni wanaokimbia na wanafunzi wanakabiliwa na ‘hatari na mateso.”
“Nina wasiwasi kuhusu ripoti zilizothibitishwa, za kuaminika za ubaguzi, ghasia na chuki dhidi ya raia kutoka mataifa yanayoendelea wanaojaribu kukimbia mzozo nchini Ukraine,” mkuu wa IOM alisema katika taarifa.
“Ubaguzi kwa misingi ya rangi, kabila, utaifa au hali ya uhamiaji haukubaliki. Ninachukizwa na vitendo vyovyote vile na kutoa wito kwa mataifa kuchunguza suala hili na kulishughulikia mara moja.”
Mataifa ya Kiafrika ya Baraza la Haki za Kibinadamu pia yalisikitishwa na ripoti za Waafrika “kunyimwa haki ya kuvuka mpaka kwenda maeneo salama.”
“Kila mtu ana haki ya kuvuka mipaka ya kimataifa wakati wa mzozo,” mwakilishi wa Ivory Coast alisema, kwa niaba ya kundi hilo.
“Onyesha usawa na uungwaji mkono kwa watu wote wanaokimbia vita, bila kujali utambulisho wao wa rangi,” alihimiza.