Jumuiya ya Afrika Magharibi ECOWAS imetangaza kutuma “kikosi cha kuweka utulivu” nchini Guinea-Bissau, ambapo jaribio la mapinduzi wiki hii lilisababisha vifo vya watu 11.
Baada ya mkutano wa kilele wa Alhamisi jioni, jumuiya hiyo ya mataifa 15 “ilishutumu vikali jaribio la mapinduzi” katika nchi hiyo yenye watu milioni mbili.
Iliongeza kuwa “kikosi cha kuweka utulivu” kitatumwa Guinea-Bissau, bila kutoa maelezo zaidi.
Urais wa Guinea-Bissau ulikataa kutoa maoni yake siku ya Ijumaa walipowasiliana na AFP.
Siku ya Jumanne, watu waliokuwa na silaha nzito walishambulia majengo ya serikali katika mji mkuu Bissau ambapo Rais Umaro Sissoco Embalo aliaminika kuhudhuria mkutano wa baraza la mawaziri.
Rais huyo mwenye umri wa miaka 49 hakujeruhiwa katika makabiliano ya risasi yaliyodumu kwa muda wa saa tano, na baadaye alielezea kuwa shambulio hilo lilikuwa ni njama ya kuiangamiza serikali.
Watu 11, wakiwemo raia wanne, waliuawa, kwa mujibu wa msemaji wa serikali.
Guinea-Bissau ni taifa ambalo limetikiswa na machafuko ya mara kwa mara, ikiwa imekumbwa na mapinduzi manne ya kijeshi tangu uhuru kutoka kwa Ureno mwaka 1974, ambayo ni ya hivi karibuni na mapinduzi ya mwaisho yakiwa mwaka 2012.
Jumuiya ya Kiuchumi ya Afrika Magharibi (ECOWAS) pia ilituma askari wa kulinda amani nchini humo mwaka 2012 kulinda majengo ya umma miongoni mwa majukumu mengine. Jeshi liliondoka wakati utulivu uliporudi mnamo 2020.
Mnamo mwaka wa 2014, Guinea-Bissau iliapa kurejesha demokrasia, lakini imekumbwa na misukosuko ya mara kwa mara tangu hapo. Watu waliohusika na jaribio hilo la mapinduzi hawajajulikana hadi sasa. Jeshi limeanzisha uchunguzi mkubwa.
Serikali ya Guinea-Bissau pia imeamuru muda wa siku mbili wa maombolezo ya kitaifa kwa waliouawa katika jaribio la mapinduzi kuanzia Jumamosi.