Raia watatu wa Marekani waliohukumiwa kifo kwa kuhusika katika jaribio la mapinduzi nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo mwaka jana wamerudishwa Marekani kutumikia kifungo.
Wiki iliyopita, Rais Felix Tshisekedi alitia saini amri ya kubatilisha hukumu ya Wamarekani hao kutoka hukumu ya kifo na kuwa kifungo cha maisha.
“Wafungwa watatu wa Marekani; Marcel Malanga Malu, Tylor Thomson na Zalman Polun Benjamin waliondoka DR Congo Jumanne kutumikia kifungo kilichosalia nchini Marekani, amesema Msemaji wa Rais wa DRC, Tina Salama.
Hatua ya kurejeshwa nyumbani imekuja baada ya Marekani na DRC kufikia makubaliano ya madini katika nchi hiyo ambapo mshauri mkuu wa Rais wa Marekani, Donald Trump Afrika alitembelea DRC na kuthibitisha kuwa nchi hizo mbili ziko kwenye mazungumzo kuhusu madini na kusema inaweza kuhusisha uwekezaji wa mabilioni ya dola.