Search
Close this search box.
Africa
Roch Kabore, Rais wa Burkina Faso

Wanajeshi nchini Burkina Faso siku ya Jumatatu walitangaza kwenye televisheni ya taifa kwamba wametwaa mamlaka katika nchi hiyo ya Afrika Magharibi kufuatia maasi yaliyotokana na kushindwa kwa rais wa kiraia kuwadhibiti waasi wa Kiislamu.

Afisa wa jeshi alitangaza kusimamishwa kwa katiba, kuvunjwa kwa serikali na bunge, na kufungwa kwa mipaka ya nchi kuanzia usiku wa manane Jumatatu, akisoma taarifa iliyotiwa saini na Luteni Kanali Paul-Henri Sandaogo Damiba.

Alisema Vuguvugu jipya la Patriotic for Preservation and Restoration (MPSR) litarejesha “uongozi wa katiba” kwa “wakati unaofaa’ akiongeza kuwa amri ya kutotoka nje usiku yote itatekelezwa.

Mamia ya watu walikusanyika kusherehekea mapinduzi ya kijeshi huko Ouagadougou, kwa kuwakaribisha wanajeshi, kupiga honi za magari na kupeperusha bendera ya taifa.

Mapema Jumatatu, mataifa yenye nguvu ya Afrika na yale ya Magharibi yalilaani kile walichokiita “jaribio la mapinduzi” na EU ilitaka “kuachiliwa mara moja” kwa Rais Roch Marc Christian Kabore.

Amerika pia ilitoa wito wa kuachiliwa kwa Kabore na kuwataka “wanachama wa vikosi vya usalama kuheshimu katiba ya Burkina Faso na uongozi wa kiraia.”

Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres alisema katika taarifa yake “analaani vikali jaribio lolote la kunyakua serikali kwa kutumia silaha”, na kuyataja matukio hayo kuwa “mapinduzi.”

Kufuatia ripoti zinazokinzana kuhusu aliko Kabore mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya Josep Borrell alisema katika taarifa yake: “Sasa tunajua kuwa Rais Kabore yuko chini ya udhibiti wa jeshi.”

Aliitaja  hali hiyo kama “inayotia wasiwasi sana”.

Chanzo cha serikali kilisema kwamba Kabore “alitolewa” nyumbani kwake Jumapili jioni na walinzi wake wa rais “kabla ya kuwasili kwa watu wenye silaha ambao walifyatulia risasi magari ya msafara wake.”

Mwandishi wa AFP mapema Jumatatu aliona magari matatu yaliyokuwa na risasi nje ya makazi ya Kabore, na michirizi ya damu kwenye gari moja.

Siku ya Jumapili, wanajeshi waliinuka katika kambi kadhaa za jeshi kote nchini Burkina Faso, ambayo imekuwa ikipambana na waasi wa Kiislamu tangu 2015.

Walidai kuondolewa kwa wakuu wa kijeshi na rasilimali zaidi za kupambana na waasi, lakini hawakutaja chochote cha kutaka kuondolewa kwa Kabore.

Kabore ni rais, ambaye amekuwa madarakani tangu 2015 na kuchaguliwa tena 2020, amekabiliwa na hasira ya umma juu ya kushindwa kukomesha umwagaji damu katika nchi hiyo.

Siku ya Jumatatu, chama tawala cha People’s Movement for Progress kilisema Kabore alikuwa mhasiriwa wa “jaribio la mauaji”.

Waziri wa serikali, ambaye hakutajwa jina, pia alinusurika katika jaribio la kumuua huku nyumba ya rais ikiporwa, kiliongeza.

Chama hicho kilisema ikulu ya rais “imezingirwa” na “kundi la watu wenye silaha” na kuwa kituo cha redio na televisheni ya taifa “kilikuwa kimetekwa”

Takriban wanajeshi 10 waliojifunika nyuso zao walitumwa mbele ya makao makuu ya shirika la utangazaji la taifa RTB siku ya Jumatatu, mwandishi wa habari wa AFP alisema.

Chanzo cha serikali kilisema Kabore “ametolewa” nyumbani kwake Jumapili jioni na walinzi wake wa rais “kabla ya kuwasili kwa watu wenye silaha ambao walifyatua risasi kwenye magari ya msafara wake.

Hapo awali, chama tawala kilihimiza “vikosi vya usalama vya nchi na wa Burkinabe wazalendo kujitenga na jaribio hilo la kuvuruga amani ya nchi na kusimama na watu wa Burkinabe, sheria na demokrasia.”

Ujumbe kwenye ukurasa wa Twitter wa Kabore uliwataka “wale ambao wamechukua silaha kuziweka chini kwa maslahi makubwa ya taifa.”

Haikuwezekana kuthibitishwa ikiwa rais aliandika tweet mwenyewe, au alilazimishwa.

Burkina Faso imeshuhudia mapinduzi kadhaa au majaribio ya mapinduzi. Katika nchi jirani ya Mali — ambako uasi ulianza wanajeshi waliiangusha serikali ya kiraia mwaka 2020.

Siku ya Jumatatu, mataifa ya Afrika Magharibi chini ya jumuiya ya ECOWAS yalielezea hali tete ya hivi punde kama “jaribio la mapinduzi” na kuwa askari watahitajika kuwajibikia usalama wa afya njema ya Kabore.

Umoja wa Afrika ulisema kuwa mkuu wa ujumbe huo, Moussa Faki Mahamat, “analaani vikali jaribio la mapinduzi dhidi ya rais aliyechaguliwa kidemokrasia.”

Ufaransa, mkoloni wa zamani nchini Burkina Faso, uliwataka raia wake nchini humo “kuepuka kusafiri” na kusema safari mbili za ndege za Air France zilizopangwa kusafiri Jumatatu jioni zimefutiliwa mbali.

Siku ya Jumapili, milio ya risasi ilisikika katika kambi nyingi za kijeshi na karibu na makazi ya Kabore mjini Ouagadougou. Mtandao ulikatwa siku hiyo hiyo.

Polisi walitumia vitoza machozi kutawanya maandamano yaliyopigwa marufuku siku ya Jumamosi, na kuwakamata watu kadhaa.

Jumapili, waandamanaji walichoma moto makao makuu ya chama tawala. Maandamano mapya yalifanyika Jumatatu.

Uasi ambao umesababisha umwagaji mkubwa wa damu ulianzia nchini Mali, na umevishinda vikosi vya Burkina vilivyo na mafunzo duni na vyenye vifaa vibaya.

Takriban watu 2,000 wamekufa, kulingana na hesabu ya AFP, wakati karibu watu milioni 1.5 ni wakimbizi wa ndani, kulingana na shirika la dharura la kitaifa CONASUR.

Comments are closed