Watu wanane walikufa maji katikati mwa Nigeria wakati mtumbwi wao ulipopinduka walipokuwa wakikimbia uvamizi wa magenge ya wahalifu, afisa wa huduma za dharura alisema Alhamisi.
Abiria hao walikuwa wakikimbia vijiji vya Guni na Kurgbaku katika wilaya ya Munya siku ya Jumatano wakati mtumbwi wao uliokuwa umejaa mizigo ulipozama kwenye mto Guni-Zumba, Ibrahim Ahmad Inga, mkuu wa wakala wa usimamizi wa dharura wa serikali ya Niger, aliiambia AFP.
“Mtumbwi huo ambao ulikuwa wa zamani ulizama kutokana na mizigo mingi na kusababisha kufa maji kwa abiria wanane wakiwemo wanawake wawili na watoto sita,” alisema.
Msako unaendelea kuwatafuta abiria wengine watano, alisema.
Ajali za boti ni za kawaida kwenya maziwa nchini Nigeria, zaidi kutokana na msongamano wa watu na ukosefu wa ukarabati wa boti hizo, hasa wakati wa msimu wa mvua.
Kaskazini-magharibi na katikati mwa Nigeria ni kitovu cha magenge ya wahalifu wenye silaha kali ambao huvamia vijiji, na kuua na kuwateka nyara wakazi baada ya kupora na kuchoma nyumba zao.
Magenge hayo ambayo yalitangazwa rasmi kuwa magaidi mwezi Januari.
Hivi majuzi wamezidisha mashambulizi yao licha ya kukabiliwa na jeshi.
Siku ya Jumatatu, majambazi walishambulia treni katika jimbo jirani la Kaduna na kuwaua abiria wanane na kuwajeruhi wengine 26.
Tukio hilo lilitokea siku mbili baada ya uwanja wa ndege wa Kaduna kushambuliwa, na kusababisha afisa wa usalama kupoteza maisha na kutatiza safari za ndege kwa muda.