Wapambe Wa Raila Wazidi Kususia Mikutano Ya Hadhara Ya Upinzani Nchini Kenya

(Picha Hisani -Simon MAINA / AFP)

Mrengo wa upinzani nchini Kenya ukiongozwa na Kinara wake Raila Odinga unazidi kukumbwa na mawimbi si haba ambayo huenda yakasababisha mgawanyiko baina ya viongozi kutoka vyama tanzu.

Mawimbi haya yameonekana wazi katika mikutano ya Azimio-Oka ya hivi majuzi ambayo wamekuwa wakiandaa katika sehemu tofauti nchini kuipa shinikizo serikali ya rais William Ruto kuangazia baadhi ya changamoto zinazowakumba wakenya ikiwemo gharama ya juu ya maisha.

Kukosekana kwa baadhi ya wapambe wa Raila katika mikutano ya hadhara kumeibua maswali mengi,huku wadadisi wa kisiasa wakidokeza kuwa hili litapanua zaidi ufa ulioko katika mrengo wa upinzani.

Kati ya kaunti sita ambazo Raila amezuru tangu kuzindua mikutano ya hadhara mwezi Januari mwaka huu,angalau magavana sita wa upinzani wamedinda kuhudhuria.

Baadhi ya magavana hao wameshaonyesha nia ya kushirikiana na serikali ya Rais William Ruto ili kupata maendeleo.

Magavana hawa ni Wavinya Ndeti wa kaunti ya Machakos, Paul Otuoma wa Busia, George Natembeya wa Trans Nzoia, Amos Nyaribo wa Nyamira na Wilber Otichilo wa kaunti ya Vihiga.

Wakati kiongozi wa upinzani Raila Odinga alipozuru kaunti ya Trans Nzoia Jumapili kwa ajili ya mkutano wa hadhara ulioandaliwa katika uwanja wa Kitale, gavana wa Trans Nzoia George Natembeya alidinda kuhudhuria,hatua ambayo viongozi wa upinzani walimpiga vijembe kwa kugura upinzani.

Natembeya alichaguliwa kwa tiketi ya chama cha DAP-K,chama tanzu ndani ya muungano pinzani Azimio-Oka.

Natembeya ni baadhi ya magavana kutoka upinzani ambao wameonyesha waziwazi nia ya kufanya kazi na Rais Willia Ruto.

“Ajenda yangu ni moja tu,kuhakikisha kuwa wananchi wa kaunti ya Trans Nzoia wanapata maendeleo. Kuhakikisha hili linaafikiwa,nipo tayari kufanya kazi na srikali ya kitaifa ikiongozwa na rais William Ruto. Nataka kuona mabadiliko katika kaunti ya Trans Nzoia,” alisema gavana Natembeya Januari 18.

“Nawaomba viongozi waliochaguliwa kuweka kando siasa za chama na kuangazia changamoto zinazowakumba wananchi waliowachagua,”alisema Natembeya.

Gavana wa kaunti ya Machakos Wavinya ndeti ambaye alichaguliwa kwa tiketi ya chama cha wiper ambacho kipo ndani ya muungano wa Azimio-Oka amejitokeza wazi wazi kudai kuwa atashirikiana na serikali kuu kufanikisha ajenda ya maendeleo kaunti ya Machakos.

Wavinya hakuonekana katika mkutano wa hadhara wa upinzani ulioandaliwa Januari 13 mjini Mavoko kaunti ya Machakos kwani alikuwa anahudhuria kikao cha magavana na Rais William Ruto eneo la Navaisha.

“Serikali yangu ya Kaunti inajizatiti kutimiza ajenda kuu ambazo iliahidi wakaazi ikiwemo afya kwa wote ambayo itafanikiwa iwapo nitashirikiana na serikali ya Rais William Ruto”alisema Wavinya.

Ikumbukwe kuwa Rais William Ruto amekuwa akiandaa vikao na viongozi kutoka mrengo wa upinzani katika ikulu Nairobi,hatua ambayo imeonekana kuukera upinzani na hata kusababisha viongozi waliohudhuria vikao hivyo kutajwa kama “waasi”.