Washindi Tuzo ya Safal ya Kiswahili ya fasihi ya Africa kujulikana Julai 3

Wakati washindi wa tuzo ya Kiswahili ya Safal ya Fasihi ya Afrika kwa tanzu za riwaya, ushairi, wasifu, tamthilia na michoro wakitarajiwa kutangazwa Julai 3, 2025, imeelezwa kuwa kiwango cha ubora wa miswada inayoshindanishwa kinaongezeka kila mwaka, lengo likiwa ni kukienzi Kiswahili.

Hayo yamesemwa leo Alhamisi Juni 26, 2025 jijini Nairobi wakati waandaaji wa tuzo hiyo wakitangaza orodha ya miswada ya mashindano ya mwaka 2024.

 

Tuzo hiyo inayofadhiliwa na Kampuni ya Safal Group, kupitia Alaf Tanzania na Mabati Rolling Mills Kenya, ilianzishwa na Dk Lizzy Attree na Dk Mukoma Wa Ngugi mwaka 2014 ili kutambua uandishi kwa lugha za Kiafrika

Na Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya Tuzo hii, Abdilatif Abdalla, amefurahishwa na jinsi Tuzo hili linaendelea kuvutia watu wengi katika mataifa mbali mbali.

“Ni jambo la kufurahisha mno kuona kwamba tangu mashindano yalipoanzishwa mwaka 2015 bado Tuzo hii inaendelea kuwavutia washiriki kutoka nchi mbalimbali na kwa idadi kubwa. Pia kiwango cha
ubora wa miswada inayoshindanishwa kinaongezeka kila mwaka, na kwa hivyo kuitajirisha Fasihi
ya Kiswahili.” alisema Abdulatif

kwa upande wake Bi Siprosa Rabach, Mkuu wa Safal MRM Foundation, alisema, “Tuzo hii si tu zawadi ya fasihi — ni ishara ya kujitolea kwa ajili ya utambulisho wa Kiafrika. Kwa kusaidia kazi asilia kwa Kiswahili,tunasaidia kulinda na kuinua lugha ambayo inaendelea kuunganisha, kuhamasisha na
kuwezesha mamilioni kote barani Afrika.

Majaji waliopitia na kuchambua jumla ya miswada 210 pamoja na Dkt. Salma Hamad ni Prof.
Richard Wafula wa Chuo Kikuu cha Kenyatta, Kenya, na Dkt. Caesar Jjingo wa Chuo Kikuu cha
Makerere, Uganda.

Washindi wa orodha hii fupi watatangazwa katika sherehe itakayofanyika tarehe 3 Julai, 2025,
jijini Dar es Salaam, Tanzania. Zawadi za jumla ya dola za Marekani 15,000 zinatolewa kwa
miswada bora zaidi ambayo haijachapishwa.

Tanzu zinazoshindaniwa ni riwaya, ushairi, wasifu,tamthilia na riwaya za michoro. washindi wa Kwanza katika  vitengo vya Riwaya na Ushairi  watapokea  Dola 5,000 na kisha washindi  wa Pili (katika utanzu wowote) watapokea Dola 2,500


Mbali na zawadi hizo, miswada itakayoshinda itachapishwa na Mkuki na Nyota Publishers,
Tanzania. Miskwada ya mashairi itatafsiriwa kwa Kiingereza na kuchapishwa na Africa Poetry

Tuzo ya Kiswahili ya Safal ya Fasihi ya Afrika hutolewa kila mwaka kwa miswada bora katika
tanzu za riwaya, ushairi, wasifu, tamthilia na riwaya za michoro. Miswada hiyo ni lazima iwe
haijachapishwa au kusambazwa kwa njia yoyote rasmi.

 

Tuzo hii inadhaminiwa na kampuni ya Safal Mauritius Limited (ikiwa na matawi yakiwemo
Mabati Rolling Mills Limited, Kenya, na ALAF Limited, Tanzania) inayojulikana kwa jina la
pamoja la The Safal Group.

Tuzo ya Kiswahili ya Safal ya Fasihi ya Afrika ilianzishwa na Dkt. Lizzy Attree na Dkt. Mukoma Wa
Ngugi mwaka 2014 ili kutambua uandishi kwa lugha za Kiafrika na kuhimiza tafsiri kutoka lugha
hizo, baina ya lugha hizo na kwa lugha hizo.