Makundi yenye silaha yamewauwa raia saba na wanajeshi watatu wa vikosi vya usalama mashariki mwa DR Congo, ambapo kliniki ilichomwa moto, duru za ndani zilisema Alhamisi.
Askari wawili wa Butembo, yapata kilomita 50 kutoka Beni katika jimbo la Kivu Kaskazini, waliuawa na “wanamgambo wa Mai-mai,” alisema Kanali Donat Mandonga, afisa mkuu wa utawala katika wilaya jirani ya Lubero.
Polisi na wanamgambo wanne pia waliuawa katika mapigano hayo, alisema Kapteni Anthony Mualushayi, msemaji wa jeshi katika eneo la Beni.
Neno “Mai-mai” linatumika sana kutambulisha vikundi vilivyojihami vinavyodai kuwakilisha jamii katika mizozo mingi ya kikabila katika eneo hilo.
Kundi la Allied Democratic Forces (ADF) liliwauwa wanawake wanne na wanaume watatu siku ya Jumatano walipokuwa wakifanya kazi katika mashamba karibu na mpaka wa Uganda, Ricardo Rupande, mratibu wa jumuiya huko Rwenzori, aliiambia AFP.
Kundi la ADF linadaiwa kuwa mfuasi wa kundi la Islamic State.
Usiku huo huo, wanachama wa ADF walichoma moto kituo cha matibabu katika kijiji cha Luonoli,chifu wa kijiji cha Luonoli Semu Kiheka aliambia AFP, akiongeza kuwa watu wa eneo hilo walikimbia baada ya shambulio hilo.
Kundi la ADF ndilo lenye kusababisha vurugu zaidi kati ya zaidi ya makundi 120 yenye silaha ambayo huzunguka mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, kulingana na wachunguzi.
Kundi hilo linatuhumiwa kuwaua maelfu ya watu katika kampeni ya miaka mingi katika eneo hilo, na kufanya mashambulizi ya hivi karibuni katika mji mkuu wa Uganda Kampala.
Mnamo tarehe 30 Novemba, wanajeshi wa Uganda walijiunga na wanajeshi wa Congo katika msako mkali dhidi ya ADF katika eneo la Beni.