Watu 12 akiwemo afisa mkuu wa jeshi wako kizuizini nchini Burkina Faso baada ya njama inayoshukiwa kuwa ya “kuvuruga taasisi za nchi” kufichuliwa wiki hii, Waziri wa Majeshi Aime Barthelemy Simpore alisema Alhamisi.
Watu 15 wamekamatwa tangu Jumatatu, wakijumuisha “maafisa wawili, maafisa saba wasio na tume, afisa mkuu na raia watano,”Jenerali Simpore alisema baada ya mkutano wa baraza la mawaziri.
Kati ya hao, raia wawili na askari mmoja wameachiwa baada ya kutoa ushahidi wa awali na kuwaacha wengine 12 kizuizini, alisema.
Simpore alisema kukamatwa kwa watu hao kuliamriwa na waendesha mashtaka katika mahakama ya kijeshi katika mji mkuu Ouagadougou kutokana na “jaribio linaloshukiwa kuwa la kuvuruga taasisi za serikali.”
Nchi hiyo ya Afrika Magharibi ina historia ndefu ya mapinduzi na inapambana na waasi wa kijihadi waliotokea nchi jirani ya Mali mwaka 2015.
Mzozo huo umesababisha vifo vya takriban watu 2,000, kulingana na hesabu ya AFP, na kuwalazimisha watu milioni 1.5 kutoroka makazi yao, kulingana na shirika la kitaifa la misaada ya dharura CONASUR.
Wachunguzi walipokea taarifa kutoka kwa askari “anayeaminika aliwasiliana na kundi la watu binafsi, (wakimtaka) kuungana nao kufanya vitendo vya kuyumbisha taasisi,” alisema waziri huyo.
“Tunaomba nchi iwe na utulivu na watu waendelee na shughuli zao huku waendesha mashtaka wakifuatilia uchunguzi wao na kutoa ripoti yao,” alisema.
Wanajeshi wanane walikamatwa siku ya Jumatatu, akiwemo afisa mkuu, Luteni Kanali Emmanuel Zoungrana, ambaye alikuwa akiongoza oparesheni za kupambana na wanajihadi katika eneo lililoathirika vibaya la magharibi mwa nchi, vyanzo vya usalama viliiambia AFP mapema wiki hii.
Moja ya vyanzo vilisema “tuhuma za njama ya kuvuruga utulivu na athari za kigeni” zilimuathiri Zoungrana na wanajeshi kadhaa tangu maandamano ya Novemba.
Mamia ya waandamanaji waliingia barabarani Novemba 27 wakipinga kushindwa kwa serikali kukomesha uasi huo.
Takriban watu 12 walijeruhiwa katika mapigano kati ya waandamanaji na polisi.
Hasira kutoka kwa umma iliongezeka baada ya watu 57 wakiwemo askari 53 kuuawa wakati mamia ya wanajihadi walipovamia kambi moja kaskazini mwa Burkina Faso mapema mwezi Novemba.
Siku ya Alhamisi, serikali ilibadilisha magavana katika mikoa minne inayopambana na wanajihadi mashariki na kaskazini mwa nchi.
Kanali wanne wa jeshi walichukua nafasi walizokuwa wakishikilia raia wawili.