Watu 28 wameuawa wakati wa majaribio ya uvamizi wa mifugo kaskazini mwa Sudan Kusini, afisa wa usalama alisema Jumanne.
Mashambulizi hayo yalitokea Jumapili na Jumatatu katika kaunti ya Leer katika jimbo la Unity, kamishna wa kaunti ya Leer Stephen Taker alisema.
Washambuliaji walikuwa vijana kutoka maeneo jirani ya kaunti za Mayendit na Koch, aliambia AFP.
“Walikuja na kutushambukia. Watu kumi wa upande wetu tayari wamekufa,” alisema na kuongeza kuwa waliouawa walikuwa wachungaji wachanga na mwanamke.
“Kwa upande wao, watu 18 wamekufa.” Mchungaji Stephen Kulang Jiech, wa kanisa la Leer Presbyterian, alisema mashambulizi yalianza Jumapili jioni na kuendelea hadi Jumatatu asubuhi.
Kisha wakaendelea tena Jumatatu alasiri.
Kaunti ya Leer ilikuwa moja wapo ya vitovu vya janga la kibinadamu ambalo liliibuka kutoka kwa vita vya wenyewe kwa wenyewe vya 2013-2018, vilivyochangiwa na ghasia na njaa.
Mgogoro huo, ambao ulimkutanisha Rais wa sasa Salva Kiir dhidi ya mpinzani wake na Makamu wa Rais wa sasa Riek Machar uliwaua karibu watu 400,000 na mamilioni ya wengine kuyahama makazi yao.
Nchi hiyo yenye watu milioni 11 imejitahidi kudumisha amani katika miaka ya hivi karibuni tangu mikataba ya amani ya 2018.
Takriban raia 72 waliuawa kati ya Februari 17 na Aprili 7 katika kaunti ya Leer, Umoja wa Mataifa umesema, huku machafuko ya kikabila yakikumba eneo hilo lenye utajiri mkubwa wa mafuta.
Taifa hilo changa zaidi duniani limekumbwa na ukosefu wa utulivu tangu kuanzishwa kwake mwaka 2011, huku Umoja wa Mataifa ukionya mapema mwaka huu kwamba nchi hiyo iko katika hatari ya kurejea kwenye mzozo.