Zaidi ya watu 30 waliuawa katika mashambulizi ya watu wanaoshukiwa kuwa wanajihadi siku ya Jumapili na Jumatatu katika jimbo la Ituri kaskazini-mashariki mwa DR Congo, shirika la Msalaba Mwekundu lilisema.
Waasi wa Allied Democratic Forces (ADF), mojawapo ya makundi yenye silaha, “waliwashambulia watu” katika vijiji viwili karibu na Komanda, kilomita 75 kusini mwa mji mkuu wa jimbo la Bunia, David Beiza, mkuu wa Msalaba Mwekundu alisema.
Pamoja na kushambulia vijiji vya Mangusu, ambako raia 17 walikufa, na Shauri Moya, ambapo tisa waliuawa, washambuliaji hao pia walilenga daraja la mto Ituri, na kuua wengine wanne, Beiza alisema.
The Kivu Security Tracker (KST), mfuatiliaji anayeheshimika, aliripoti baadaye kwenye Twitter “angalau raia 18 waliuawa katika kijiji cha Mangusu… siku ya Jumatatu” na kuongeza kuwa “ADF wanashukiwa kwa mauji hayo.”
Kikundi cha ufuatiliaji hakikutaja idadi yoyote ya wale waliouawa kutoka kijiji cha Shauri Moya.
“Tangu jana, tumesikia milio ya risasi nyepesi na nzito ikitoka kwa Mangusu na Shauri Moya,” alithibitisha Daniel Herabo, kiongozi wa jumuiya ya kiraia katika eneo hilo.
Kulingana na Herabo, waasi hao waliingia kwanza Shauri Moya siku ya Jumapili na kisha Mangusu Jumatatu asubuhi.
“Huko, miili ya baadhi ya wahanga 17 ilikuwa imefungwa, wengine kukatwa shingo na wengine kuuawa kwa kupigwa risasi,” alisema Herabo ambaye hajatembelea vijiji hivyo, lakini akiwategemea wenzake katika eneo hilo.
Alisema mapigano kati ya ADF na FARDC (majeshi ya DRC) yaliendelea Jumatatu mchana.
Waasi wa ADF, ambao wanafungamana na kundi la Islamic State kama mshirika wake wa Afrika ya kati, wamehusika na ghasia kali dhidi ya raia — mara nyingi kwa mapanga na silaha nyinginezo.
Vijiji vilivyoshambuliwa viko kilomita 12 tu kutoka mji wa Drakpa ambapo raia 14, wakiwemo watoto saba, waliuawa katika kambi ya watu waliokimbia makazi siku zilizopita.
Ituri na mkoa jirani wa Kivu Kaskazini kwa sasa wako chini ya hali rasmi ya kuzingirwa, iliyotangazwa Mei mwaka jana.
Chini yake, viongozi wa kiraia wamebadilishwa na maafisa wa jeshi au polisi, kwa lengo lililotangazwa la kuongeza juhudi za kukabiliana na vikundi vyenye silaha.
Hatua hiyo hadi sasa imeshindwa kuleta amani katika eneo hilo.