Uchaguzi mkuu nchini Kenya mwaka huu wa 2022 ulipelekea baadhi ya watu maarufu kujaribu bahati yao katika nyadhifa mbalimbali.
Hata hivyo ni wachache tu ambao walifanikiwa kuibuka washindi katika nafasi ambazo walikuwa wanawania.
Baadhi ya ma-Celebs waliofanikiwa kupenya na kupata kura ya kutosha:
Mtangazaji na mwigizaji Felix Odiwour maarufu kama Jalang’o amepewa nafasi ya kuwakilisha wakaazi wa eneo bunge la Langat katika bunge la kitaifa.
Jalang’o alimshinda mbunge anayendoka Nixon Korir ambaye alikubali kushindwa hata kabla ya Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) kutangaza matokeo hayo.
Baadaye Jalang’o alitangazwa kuwa mshindi alipojizolea kura 38,948 dhidi ya Korir ambaye alipata kura 36,836.
Kabla ya kuwa maarufu Jalang’o alikuwa mvuvi katika kaunti ya Homa Bay.
“ Nikiwa na umri ya miaka 23, nilikuwa mvuvi na muuza samaki kaunti ya Homa Bay, Tungeenda hadi katikati ya ziwa usiku na kuanza shughuli za uvuvi. Nilizaliwa katika familia isiyo na mapato na wakati mwingine tungejipata hatuna chakula.” Jalang’o alisema.
Katibu mkuu wa Sportpesa Ronald Karauri sasa ndio mbunge mteule wa eneo bunge la Kasarani baada ya kutia kibindoni kura 32,406 na kumshinda John Njoroge na Mercy Gakuya ambao walipata kura 32,406 na 24,790 mtawalia.
“Alichokifanya Mungu hakuna binadamu anaweza kutenda. Ni mwamko mpya Kasarani. Sasa kazi ianze. Captain Ronald Karauri-mbunge mteule Kasarani,” Aliandika Karauri katika mtandao wa twita.
Aliyekuwa mtangazaji katika shirika la utangazaji la kitaifa (KBC) Naisula Leesuda amehifadhi kiti chake cha Samburu magharibi. Safari ya Lesuuda ya kisiasa ilianza mwaka wa 2013 wakati alipoteuliwa kuhudumu kama seneta nchini Kenya na kuwa mwanamke wa kwanza kuteuliwa kuwa mbunge kutoka kaunti la Samburu.
Mwanablogu mwenye utata Robert Alai pia ameibuka kidedea na kuwa mwakilishi wadi ya Kileleshwa kupitia chama cha Orange Democratic Movement (ODM).
Alai mwenye umri wa miaka 43, aliwabwaga wagombea wengine wanane baada ya kupata kura 638 dhidi ya mgombea wake wa karibu Junior Tollo ambaye alipata kura 545.
Mtangazaji maarufu nchini Kenya David Ngibuini anayejulikana na DNG, pia ameshinda wadhifa wa mwakilishi wadi wa Woodley, Kenyatta Golf Course.
DNG ambaye alimnia kupitia chama cha UDA chini ya muungano wa Kenya Kwanza alimshinda mwakilishi wadi anayeondoka Mwangi Njihia wa chama cha Jubilee.
Ikumbukwe kabla ya kuchaguliwa kwake DNG amekuwa mtangazaji wa televisheni, radio na pia amekuwa mfawidhi ama mshehereshaji wa hafla mbalimbali.
Akizungumza alipoonyesha ari yake ya kuingia katika siasa, DNG alisema kuwa siasa sit tu kuwa rais, gavana ama mbunge jinsi wengi wanadhani ila ni chochote ambacho kinaathiri maisha ya binadamu.
“Kitu kimoja ninachoambia kila mtu na nimeulizwa swali hili kila ninapokwenda. Watu wanadhani kwamba siasa ni tu pale ambapo unakuwa rais , gavana ama mjumbe, la hasha siasa inahusu kila kitu. Jinsi tunavyoongozwa vibaya, kwa hivyo tunapozungumzia kuhusu uongozi mbaya, viongozi wabaya tayari tupo kwenye siasa.” Alisema DND
Mwingine aliyefaulu kuingia katika siasa ni mwanamziki wa kufokafoka Eko Dyddaambaye ndiye mwakilishi wadi ya Mathare Kaskazini.
Eko Dydda alipigiwa kura kama mwakilishi (MCA) mpya katika wadi ya Mathare Kaskazini baada ya shindano la kupigilia msumari lililomshindanisha na mpinzani wake Oscar Lore.
“Nawapongeza wote walionipigia, kura zenu zilinipa ushindi wa kishindo #MCAmathareNORTH,” aliandika kwenye mitandao ya kijamii baada ya ushindi huo.
Wakati akisherehekea ushindi huo, mwanamuziki huyo alifichua kuwa amewashinda washindani wake kwa tofauti kubwa.