Takriban watu sita waliuawa katika mji mkuu wa Somalia Alhamisi katika shambulio la bomu la kujitoa mhanga lililodaiwa kutekelezwa na wanajihadi kwenye mgahawa karibu na kituo cha ukaguzi cha usalama kuelekea ikulu ya rais, afisa wa usalama alisema.
“Eneo hilo lilikuwa na watu wengi wakati mlipuko ulipotokea na baadhi ya wahasiriwa, wengi wao raia, wamejeruhiwa vibaya,” afisa wa usalama Abdullahi Muktar aliambia AFP.
Watu sita walifariki na 12 kujeruhiwa.
Huduma ya ambulensi ya Mogadishu ya Aamin ilithibitisha vifo hivyo katika taarifa iliyotumwa kwa waandishi wa habari, likisema shambulio hilo limejeruhi 13.
“Mlipuko huo ulikuwa mkubwa, na niliona ambulensi zikiwa zimebeba waathiriwa waliojeruhiwa, baadhi yao wakiwa na majeraha mabaya,” shuhuda Mohamed Tahlil alisema.
Kundi la wanamgambo wa Al-Shabaab lilidai kuhusika na shambulio hilo la kujitoa mhanga, likisema lililenga basi lililokuwa likisafirisha wajumbe wa uchaguzi ambalo lilikuwa likipitia eneo hilo wakati shambulio hilo lilipotokea.
Mogadishu imeshuhudia mfululizo wa mashambulizi katika wiki za hivi karibuni huku Somalia ikiyumba katika mzozo wa kisiasa unaosababishwa na kutoelewana kwa muda mrefu kuhusu kufanyika kwa uchaguzi.
Rais wa Somalia na waziri mkuu wamekuwa wakizozana kuhusu mchakato wa uchaguzi ambao umechelewa kwa zaidi ya mwaka mmoja na ambao umekumbwa na ghasia.
Uchaguzi wa Somalia unafuata mtindo tata usio wa moja kwa moja, ambapo mabunge ya majimbo na wajumbe wa koo huchagua wabunge wa bunge la kitaifa, ambao nao huchagua rais.
Upigaji kura kwa baraza la juu ulihitimishwa mwaka jana, wakati wajumbe wa koo hadi sasa wamechagua karibu asilimia 40 ya wabunge 275 wanaoketi katika baraza la chini.
Mgogoro huo wa uchaguzi umewatia wasiwasi waungaji mkono wa kimataifa wa Somalia, ambao wanahofia kuwa unaweza kuhatarisha vita dhidi ya Al-Shabaab, kundi la wanajihadi lenye uhusiano na Al-Qaeda ambalo limekuwa likipigana na serikali kuu dhaifu kwa zaidi ya muongo mmoja.
Siku ya Jumanne, Waziri wa Mambo ya Nje wa Amerika Antony Blinken alitangaza uamuzi wa kuzuia hati za usafiri kwa maafisa wa sasa au wa zamani wa Somalia au wengine “wanaoaminika kuhusika, au kushiriki katika, kuhujumu mchakato wa demokrasia nchini Somalia.”
Wapiganaji wa Al-Shabaab walifurushwa Mogadishu mwaka 2011 baada ya mashambulizi ya kikosi cha Umoja wa Afrika, lakini bado wanadhibiti maeneo makubwa ya vijijini Somalia ambako wanaanzisha mashambulizi ya mara kwa mara katika mji mkuu na kwingineko.