Takriban watu watano wamefariki dunia baada ya jengo kuporomoka katika kitovu cha kiuchumi nchini Ivory Coast Abidjan, huduma za dharura zilisema Jumatatu, ikiwa ni tukio la pili la aina hiyo ndani ya wiki moja.
Wazima moto walisema mwathiriwa mwingine amepatikana, na kufanya idadi ya waliofariki kufikia watano, huku 13 wakijeruhiwa.
“Operesheni zinaendelea” kuwatafuta waathiriwa wengine, zima moto walisema kwenye ukurasa wao wa Facebook.
Jengo hilo la orofa nne liliporomoka usiku wa Jumapili katika wilaya ya Angre, ambako kumeshuhudiwa ujenzi wa majumba mengi ya biashara na makazi katika miaka ya hivi karibuni.
Waziri Mkuu Patrick Achi alitembelea eneo hilo, na kuomboleza na familia za waarhiwa wa mkasa huo.
“Uchunguzi umeanza. Sheria itatumika na wenye jengo wataadhibiwa” alisema.
Mnamo Februari 27, jengo lililokuwa likijengwa liliporomoka katika sehemu nyingine ya Abidjan, na kusababisha vifo vya watu saba.