Watu watano waliuawa Jumatatu wakati basi dogo katika eneo la kaskazini-mashariki mwa Kenya kulipuliwa na bomu lililotegwa kando ya barabara wakati wa shambulizi la watu wenye silaha karibu na mpaka wa Somalia, polisi walisema.
Washambuliaji walilifyatulia risasi gari hilo baada ya kukanyaga kilipuzi takriban kilomita nane kutoka mji wa Mandera kwenye mpaka wa Kenya na Somalia.
“Kikosi cha kupiga doria cha Kitengo cha General Service, ambacho kilikuwa karibu na eneo hilo, kiliwakabili washambuliaji, ambao walikimbia kuelekea upande wa mpaka wa Somalia,” ripoti ya polisi kuhusu tukio hilo ilisema.
Washambuliaji walitumia bunduki na maguruneti ya kurushwa kwa roketi wakati wa shambulio hilo, iliongeza ripoti hiyo.
Abiria kadhaa walinusurika katika shambulio hilo “wakiwa na majeraha ya viwango tofauti”
Mkoa wa Mandera unakabiliwa na uvamizi katika mpaka wake na Somalia, ambapo wanamgambo wa Al-Shabaab wanadhibiti maeneo mengi ambapo usalama ni dhaifu.
Mikoa mingine inayopakana na Somalia pia hushambuliwa na wanajihadi na maafisa wa Kenya mara nyingi huwa wepesi kuwalaumu wanamgambo hao kwa mashambulizi katika ardhi yake.
Kenya imekumbwa na mashambulizi kadhaa mabaya ya wapiganaji wa Al-Shabaab. Mashambulizi hayo yakiwa ya kulipiza kisasi kwa Nairobi kutuma wanajeshi wake Somalia mwaka 2011 kama sehemu ya kikosi cha Umoja wa Afrika kuwatimua wanajihadi nchini Somalia.
Kenya hupeleka wanajeshi katika Misheni ya Umoja wa Afrika nchini Somalia (AMISOM).
Mnamo 2015, shambulio katika chuo kikuu cha Garissa, mkoa mwingine ulio mpakani na Somalia, lilisababisha vifo vya watu 148, karibu wote wakiwa wanafunzi.
Wengi wao walipigwa risasi baada ya kutambuliwa kuwa Wakristo.
Wiki iliyopita, balozi kadhaa za kidiplomasia mjini Nairobi zilionya juu ya uwezekano wa shambulio la kigaidi linalolenga raia wa kigeni mjini humo.
Balozi za Ufaransa na Ujerumani zilionya kuhusu uwezekano wa kutokea shambulio ndani ya siku chache, huku Amerika ikitoa onyo jipya la tahadhari kuhusu uwezekano wa kutokea kwa vitendo vya vurugu wakati huu nchini Kenya.
Mnamo mwaka wa 2019, Al-Shabaab waliwaua watu 21 katika hoteli moja ya kifahari jijini Nairobi, na mwaka wa 2013 shambulizi jingine lilitokea katika jumba la maduka la Westgate ambapo watu 67 waliuawa.