Wavamizi nchini Mali waliwauwa takriban raia 20 katika mashambulizi kwenye vijiji karibu na mji wa kaskazini wa Gao mwishoni mwa juma, huku bomu la kutegwa ardhini likimuua mlinda amani wa Umoja wa Mataifa katika eneo hilo lenye machafuko.
“Magaidi siku ya Jumamosi waliwaua takriban raia 20 katika vitongoji kadhaa katika eneo la Anchawadj, kilomita chache kaskazini mwa Gao, alisema afisa mkuu wa polisi ambaye aliomba kutotajwa jina.
Afisa mmoja wa eneo hilo alilaumu mashambulizi hayo kwa wanajihadi na kusema idadi ya waliouawa walikuwa 24, akisema mauaji hayo yalitokea Ebak, takriban kilomita 35 kaskazini mwa Gao, mji mkuu wa mkoa huo.
Hali katika Anchawadj ilikuwa ya kusikitisha sana na raia walikuwa wakikimbia eneo hilo wakihofia ghasia zaidi, aliongeza.
Kufuatia umwagaji damu siku ya Jumamosi, bomu lililotegwa ardhini lilimuua mlinda amani wa Umoja wa Mataifa siku ya Jumapili alipokuwa akipiga doria zaidi kaskazini mwa Kidal, mkuu wa kikosi cha Umoja wa Mataifa cha MINUSMA cha Mali, El Ghassim Wane, alitweet.
Msemaji wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres alilaani mauaji ya mlinda amani huyo ambaye alisema alikuwa akitokea Guinea.
“Mashambulizi yanayowalenga walinda amani wa Umoja wa Mataifa yanaweza kujumuisha uhalifu wa kivita chini ya sheria za kimataifa,” aliongeza msemaji huyo.
Ingawa kumekuwa hakuna uthibitisho rasmi kwamba mashambulizi hayo yalifanywa na makundi ya kijihadi, wapiganaji walio na mafungamano na Al-Qaeda au kundi la Islamic State wanafanya kazi katika eneo hilo.
Eneo hilo limezidi kuwa na vurugu na kutokuwa na utulivu tangu waasi wanaotaka kujitenga wa Tuareg walipoibuka dhidi ya serikali mwaka 2012.
Wapiganaji wa kijihadi walichukua fursa ya uasi wao kuanzisha mashambulizi yao wenyewe, wakitishia mji mkuu Bamako kusini hadi jeshi linaloongozwa na Ufaransa likawarudisha nyuma mwaka wa 2013. Waasi wa Tuareg na serikali walikubaliana kufikia makubaliano ya amani mwaka 2015, lakini bado makubaliano hayo hayajatimizwa.
Kwa hivyo sasa serikali dhaifu, ya kitaifa ya Mali inakabiliwa na waasi wanaotaka kujitenga na wanajihadi kaskazini mwa nchi — eneo kubwa la jangwa ambalo halina miundombinu.
“Eneo la Gao na lile ya Menaka” yanakaliwa na wanajihadi, alisema afisa huyo huko Gao.
Baadhi ya makundi ya waasi pia yamekuwa yakipigana wenyewe kwa wenyewe huku wakipigania ushawishi na maeneo.
Wanaochangia kwa hali tete ni wafanyabiashara haramu na vikundi vingine vya uhalifu.
Uthabiti wa serikali wakati huo huo umekatizwa na mapinduzi ya kijeshi mnamo Agosti 2020 na Mei 2021.
Kufuatia ripoti yake ya hivi punde kuhusu eneo hilo, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres mwezi uliopita alionya kwamba ukosefu wa utulivu nchini Mali na Burkina Faso unadhoofisha majaribio ya kuleta utulivu katika eneo hilo.
Hali ya usalama katika eneo la Gao ilikuwa imezorota vibaya katika miezi ya hivi karibuni, alisema.
Pia alionyesha wasiwasi wake kuhusu Menaka, eneo la mashariki linalopakana na Niger.
Hapo awali ilitekwa na kundi la waasi la Tuareg muongo mmoja uliopita, na baadaye kutekwa na vikundi vya Kiislamu.