Jua la alasiri linapoanza kuzama katikati mwa Kenya, mji wa Maua huwa na shughuli nyingi wakati mavuno ya mirungi yanapowasili.
Kwa miongo kadhaa, zaidi ya watu nusu milioni katika eneo hili wameishi kwa kutegemea mirungi, mti pia unaojulikana kama miraa.
Kila siku miraa huunganishwa na kufungwa kwenye majani ya migomba, hupakiwa kwenye mifuko na kupakiwa kwenye lori.
Kisha madereva husafirirsha bidhaa hiyo kwa barabara kwa mwendo wa kasi katika juhudi za kuhakikisha kwamba miraa ni mbichi inapowafikia watumiaji kaskazini na mashariki mwa Kenya, pamoja na mji mkuu wa Nairobi, ulioko kilomita 300 kutoka Meru.
Lakini kwa miaka miwili iliyopita, hakuna shehena ya miraa iliyosafirshwa kwa anga kutoka ya Kenya kwenda Somalia.
Somalia ni nchi isiyokuwa na utulivu lakini bado ni mojawapo ya soko kubwa la miraa, ambayo hutafunwa ili kutoa kichocheo na kukandamiza hamu ya kula.
Hapo awali Mogadishu ilipiga marufuku shehena za anga mnamo Machi 2020 kutokana na janga la UVIKO 19, lakini mvutano wa kidiplomasia kati ya Kenya na Somalia umeweka marufuku hiyo hata baada ya vizuizi vingine vya UVIKO-19 kuondolewa.
Kuchaguliwa kwa Rais Hassan Sheikh Mohamud nchini Somalia mwezi uliopita kuliibua matumaini ya kuboreshwa kwa uhusiano na Nairobi, na Juni 10, Waziri wa Kilimo wa Kenya Peter Munya alitangaza kwamba Mogadishu ilikubali kurejesha usafirishaji wa anga wa miraa.
Habari hizo zimezua msisimko huko Maua, ambapo wamekuwa wakisubiri mabadiliko.
Ingawa Munya aliahidi kwamba usafirishaji wa anga utaanza tena ndani ya wiki mbili, serikali mpya ya Somalia imedumisha ukimya juu ya suala hilo.
“Kurejeshwa kwa biashara itakuwa kama kuzaliwa upya” kwa eneo hilo, alisema Kimathi Munjuri, mwenyekiti wa Chama cha Wafanyabiashara wa Miraa cha Nyambene katikati mwa Kenya.
Lakini aliendelea kuwa makubaliano kama hayo hapo awali hayakutimia.
Kabla ya kupigwa marufuku, karibu theluthi moja ya tani 150 za miraa zinazosafirishwa kila siku zilikwenda Somalia, ikiwakilisha hasara ya mapato ya hadi shilingi milioni 16 za Kenya (dola 136,000), alisema.
Somalia imekuwa soko muhimu la uuzaji wa nje wa miraa nchini Kenya tangu Uholanzi na Uingereza zilipoweka marufuku mwaka wa 2012 na 2014 mtawalia, ikijiunga na mataifa mengine ya Magharibi ambayo yalijumuisha bidhaa hiyo kama dawa ya kulevya.
Mkulima wa miraa David Muchoka ni miongoni mwa wale wanaotamani kuona kurejeshwa kwa usafirishaji wa anga kwenda Mogadishu.
Marufuku hiyo ilisababisha mapato yake kushuka, alisema, na kumlazimisha baba wa watoto sita kujitosa katika ufugaji wa ng’ombe wa maziwa ili kulipa bili.
“Hapo zamani tungeweza kutengeneza hadi shilingi 100,000 ($850) kwa mwezi mmoja, lakini sasa tunaweza tu kutengeneza takriban 6,000-10,000 kwa mwezi,” mwanamume huyo mwenye umri wa miaka 53 aliiambia AFP.
“Bado tunauza miraa lakini kwa hasara, mapato hayawezi kuendeleza juhudi za kukuza shamba na kulipa karo za shule.”
Mapato kutokana na biashara hiyo yalikuza biashara katika eneo zima, wenyeji waliiambia AFP.
“Maduka mengi ya hapa yamefungwa, magari yaliyokuwa yakisafirisha miraa hayafanyi kazi, watu wengi hawawezi tena kupeleka watoto wao shule,” alisema Alex Koome, mkazi wa Maua.
Watu wengi hapa wanasubiri ile siku ambapo Maua itakuwa tena katika msisimko wa biashara ambayo ilihuisha jiji saa 24 kwa siku.
“Maua ilikuwa hailali… Tunataka ule uchangamfu, ule msukumo,” Munjuri aliiambia AFP huku akitabasamu.
Kwa Joseph M’Eruaki, mkurugenzi wa zamani wa maendeleo ya kijamii katika shirika lisilo la faida la Caritas katika Kaunti ya Meru, ambako Maua iko, marufuku hiyo imefichua utegemezi hatari wa miraa.
“Lazima tubadilishe vyanzo vya riziki kama hatutaki watu kubaki katika mazingira magumu,” alisema, akipendekeza kuwa wakulima badala yake wanaweza kulima mazao kama vile mchicha, mtama, maembe au parachichi.
Mjasiriamali huyo, ambaye sasa anagombea ubunge katika uchaguzi wa Agosti nchini Kenya, pia anapigania uangalizi zaidi wa udhibiti wa biashara ambayo inajivunia sifa mbaya wakati mwingine.
“Miraa inadhibitiwa na watu wachache wanaopata faida nyingi kwa gharama ya wakulima… Wanadhibiti soko, wanadhibiti bei, wanadhibiti mtiririko, ni sawa na ukiritimba,” alisema.
“Ni zao halali, linahitaji kupangwa. Kama sekta ya chai au sekta ya kahawa,” alisema.