Wazee kutoka miji kadhaa wametoa wito wa kususia uchaguzi wa rais na waandamanaji wamefunga vituo vya kupigia kura magharibi mwa Libya siku ya Jumatatu 15 Novemba baada ya mwanawe aliyekuwa dikteta Muammar Gadhafi kujiandikisha kugombea kiti cha urais katika uchaguzi unaotarajiwa kufanyika Desemba 24.
Mwendesha mashtaka wa kijeshi nchini humo Mohamed Gharouda pia ametaka mamlaka ya uchaguzi kusitisha utayarishaji wa karatasi za ugombea urais wa Seif al-Islam Gaddafi
Seif al-Islam Gadhafi amekuwa mafichoni kwa miaka mingi asijulikane alikokuwa akiishi, hadi alipojitokeza siku ya Jumapili na kujisajili kama muaniaji wa kiti cha urais.
Baraza la wazee wenye ushawishi mkubwa kutoka Misrata, jiji ambalo lilichangia pakubwa katika uasi wa 2011 ambao ulimwondoa babake madarakani lilitoa wito wa kususia uchaguzi.
Baraza hilo katika taarifa yake lilisema kuwa “linawakataa wagombea waliotumia nguvu kupita kiasi wakati wa ukandamizaji wa kikatili dhidi ya uasi dhidi ya uongozi wa babake Muammar Gadhafi na ambao wanatakiwa na mahakama za Libya na Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu ICC’.
Mwanachama wa tume ya uchaguzi ya HNEC amesema kuwa wakaazi wanaopinga ugombezi wa Seif al-Islam Kadhafi katika uchaguzi wa urais wamefunga vituo kadhaa vya kupigia kura magharibi mwa nchi hiyo.
Huu ni uchaguzi wa kwanza wa urais kufanyika nchini Libya huku Umoja wa Mataifa ukijaribu kumaliza muongo mmoja wa ghasia tangu uasi uliomwondoa babake Gadhafi madarakani mwaka wa 2011.
Seif al-Islam angali anasakwa na Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu ICC kwa tuhuma za uhalifu wa kivita uliofanywa mwaka 2011.
Lakini Tume ya Uchaguzi ya HNEC imesema “amekamilisha masharti yote ya kisheria”ili kugombea kiti cha urais.
Siku ya Jumapili, watu mashuhuri kutoka magharibi mwa mji wa Zawiya walikataa kabisa Gadhafi na mbabe wa kivita Khalifa Haftar,ambaye pia anapanga kuwania kiti cha urais kushiriki katika uchaguzi huo.
Bw Haftar, ambaye anaongoza majeshi mashariki mwa Libya, anasakwa na mahakama ya Marekani kwa madai ya kuwatesa Walibya wakati wa vita.
uchaguzi wa Desemba 24 unapingwa na baadhi ya watu wanaodai kuwa hakuna makubaliano juu ya misingi ya kisheria na nguvu ambazo rais atakuwa nazo baada ya kuja madarakani.
Khaled al-Meshri, mkuu wa Baraza Kuu la Serikali la muda, ametoa wito wa kuahirishwa kwa uchaguzi huo akisema una ‘kasoro’ na ‘ni haramu’
Tume ya uchaguzi HNEC imesema takriban wapiga kura milioni 2.83 wamejiandikisha kupiga kura katika uchaguzi wa urais na ubunge unaotarajiwa kufanyika Desemba 24.