Waziri wa biashara wa Kenya Moses Kuria yuko katikati ya dhoruba kutokana na msururu wa matamshi ya dharau dhidi ya chombo kikuu cha habari, ikiwa ni pamoja na kuwaita waandishi wake “makahaba”.
Vyama vya upinzani na wanahabari vimetaka Moses Kuria kukemewa kutokana na miripuko yake ikisema kuwa hafai kushikilia nyadhifa za umma.
Hasira zilizuka wakati Kuria alipofanya mashambulizi dhidi ya Nation Media Group (NMG), chombo kikuu cha habari Afrika Mashariki kinachomilikiwa na Aga Khan.
Katika hafla ya hadhara Jumapili, Kuria alitishia maafisa wa serikali waliotangaza na NMG kuwafuta kazi na kuuliza chombo hicho ikiwa ni jumba la habari “au chama cha upinzani.”
“Idara yoyote ya serikali ninayoona imetangazwa kwenye Nation Media (majukwaa), jione umefukuzwa kazi,” alisema.
Katika ujumbe wake kwenye Twitter uliochapishwa kwa Kiswahili, aliwataja kama “Washerati huko Aga Khan.”
“Washerati wa Aga Khan. Muwe na usingizi poa,” ujumbe huo ulisema.
Pia alidai kuwa waandishi wa habari wa NMG “wamekiri kulazimishwa kuandika habari dhidi ya serikali na wahariri na wasimamizi wao katika mpango uliofadhiliwa na rais wa zamani.”
NMG ilisema kuwa ghasia hizo zilifuatia uchunguzi uliopeperushwa Jumapili na kituo chake cha NTV kuhusu kashfa kuhusu mpango wa uagizaji bidhaa unaoendeshwa na shirika la serikali katika wizara ya Kuria.
“Shambulio la maneno lisilo na msingi la Kuria, sio tu kwamba halikuwa na heshima kwa afisa wa serikali wa aina yake, lakini shambulio dhidi ya uhuru wa vyombo vya habari, msingi wa demokrasia,” Daily Nation ilisema katika tahariri iliyochapishwa kwenye tovuti yake Jumanne.
Seneta wa upinzani Edwin Sifuna aliwasilisha ombi la kumshutumu Kuria wiki hii, akionya kwamba shambulio dhidi ya chombo kimoja cha habari “mara nyingi husababisha mashambulizi dhidi ya uhuru wa wanahabari kwa ujumla.”
Wanachama wa muungano wa kinara wa upinzani Raila Odinga walitoka nje ya Seneti Jumatano wakilalamikia kujitokeza kwa Kuria katika ukumbi wa bunge na kukataa kwa spika kuwaruhusu kumhoji.
Kuria aliwaambia wanahabari Jumatano: “Siombi msamaha.”
Vyama vya habari vimejibu kwa hasira kutokana na maoni ya waziri huyo, ambaye alikuwa amechukua nafasi kubwa siku ya Jumatatu wakati wa kusainiwa kwa makubaliano makubwa ya kibiashara na Umoja wa Ulaya.
Muungano wa Wanahabari wa Kenya (KUJ) ulisema “anakuwa ishara ya aibu ya kitaifa” huku mdhibiti wa tasnia ya Baraza la Vyombo vya Habari nchini Kenya akisema matamshi yake ni “tishio la uhuru wa vyombo vya habari na kuharibu taswira ya Kenya duniani kote”.
Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi ya Kenya pia iliingia kwenye kinyang’anyiro hicho, ikisema hakuna mashirika ya umma ambayo “yatadhulumiwa” kwa kujihusisha na shughuli halali na shirika lolote.
Chama cha Wamiliki wa Vyombo vya Habari nchini Kenya kilisema kelele zake “zinamnyima sifa ya kushikilia wadhifa wa umma.”
Ruto amewahi kuvishutumu vyombo vya habari vya Kenya kwa kuwa na upendeleo dhidi yake, na wakati wa kampeni za uchaguzi wa Agosti 2022 alitishia kujiondoa kwenye mjadala wa urais akisema amekuwa akiripotiwa vibaya.