Msumbiji siku ya Alhamisi ilimhukumu waziri wa zamani kifungo cha miaka 16 jela kwa ufisadi, hukumu ya kushangaza kwa nchi hiyo ambayo bado inashughulika na kashfa tofauti ya ubadhirifu.
Maria Helena Taipo, 60, mwanachama wa chama tawala cha FRELIMO ambaye aliongoza wizara ya Leba kutoka 2005 hadi 2014, alishtakiwa kwa ubadhirifu wa metical milioni 113 (dola milioni 1.7) za serikali ili kujenga nyumba na kulipia gharama zingine za kibinafsi.
Maafisa wengine wanane wa serikali walihukumiwa kifungo cha kati ya miaka 12 hadi 16 katika kesi hiyo.
Hakimu wa Maputo Evandra Uamasse alisema katika kutoa hukumu kwamba, “wakiendeshwa na tamaa ya kupata faida,” washtakiwa walivunja imani ya umma.
“Mahakama inatakiwa kuwa na mtazamo wa uthabiti na ukali ili kukomesha tabia hii ,”Uamasse alisema.
Wakili wa Taipo Inacio Matsinhe alisema waziri huyo wa zamani atakata rufaa dhidi ya uamuzi huo.
Msumbiji bado haijapata nafuu kutokana na kashfa ya rushwa ya dola bilioni 2 iliyoitumbukiza nchi hiyo katika mgogoro mbaya zaidi wa kiuchumi tangu uhuru wake kutoka kwa Ureno miongo minne iliyopita.
Ikiorodheshwa miongoni mwa mataifa maskini zaidi duniani, Msumbiji ilikopa pesa kinyume cha sheria mwaka 2013 na 2014 kutoka kwa benki za kimataifa ili kununua meli za uvuvi wa tuna na meli za uchunguzi.
Serikali ilificha mikopo hiyo kutoka kwa bunge lakini deni hilo lilifichuka mwaka wa 2016, na kusababisha wafadhili kukatiza usaidizi wa kifedha.