Mkuu wa Shirika la Afya Duniani alisema Ijumaa kuwa athari kubwa ya janga la UVIKO 19 linaweza kumalizika mwaka huu, ikiwa asilimia 70 ya watu wote duniani watapata chanjo.
“Matarajio yetu ni kwamba awamu kali ya janga hili itaisha mwaka huu, bila shaka kwa sharti moja, iwapo tutatimiza lengo la kuwachanja watu asilimia 70 kufikia katikati ya mwaka huu karibu Juni, Julai,” Tedros Adhanom Ghebreyesus, aliwaambia waandishi wa habari nchini Afrika Kusini.
“Ikiwa hilo litafanyika, awamu kali inaweza kuisha, na hilo ndilo tunalotarajia. Sio suala la kubahatisha.”
Alikuwa akizungumza alipozuru maabara ya Afrigen Biologics and Vaccines, ambayo yametoa chanjo ya kwanza ya mRNA iliyotengenezwa Afrika kwa kutumia utaratibu wa Moderna.
Chanjo itakuwa tayari kwa majaribio ya kimatibabu mnamo Novemba, na kibali kinatarajiwa mwaka wa 2024.
Afrigen inaongoza mradi wa majaribio, ikiungwa mkono na WHO na mpango wa COVAX.
Kituo cha mafuzno kilianzishwa mwezi wa Julai na kitatoa mafunzo ya kuzalisha chanjo kwa nchi nyingine na kutoa leseni za uzalishaji kwa mataifa maskini yaliyoachwa katika kinyang’anyiro cha kuzalisha chanjo hizo.
Tedros alisema WHO “imejitolea kusaidia maendeleo ya viwanda vya barani Afrika na duniani kote, ili kuongeza usalama wa afya wa kikanda.”
– Idadi ya maambukizi inapungua kote duniani
Asilimia 11 ya Waafrika wamechanjwa, kiwango cha chini zaidi duniani. Wiki iliyopita ofisi ya WHO barani Afrika ilisema bara lazima liongeze kiwango cha chanjo ili kufikia lengo la asilimia 70.
Dunia iliingiwa na hofu mwishoni mwa mwaka jana kufuatia kuzuka kwa kirusi cha Omicron kilichokuwa kikiambukiza kwa kasi sana na kuongeza idadi ya maabukizi mara nne zaidi.
Lakini baada ya kuenea kwa kasi kwa kipindi cha miezi mitatu na nusu, idadi ya visa vya maambukizi mapya ya kila siku duniani ilipungua kwa wiki ya pili mfululizo, ikipungua kwa asilimia 17, kulingana na hesabu ya AFP siku ya Alhamisi.
Waziri wa Ushirikiano wa Maendeleo wa Ubelgiji, Meryame Kitir, ambaye alikuwa sehemu ya timu iliyotembelea Cape Town, alisikitishwa na maendeleo ya polepole katika mazungumzo ya kutaka kuondolewa kwa vibali vya kuzalisha chanjo.
Afrika Kusini na India tangu Oktoba 2020 zimeongoza wito wa kuondolewa kwa haki miliki ya kuzalisha chanjo, kwenye chanjo za Covid-19 zikisema hii itasaidia kuchochea uzalishaji wa ndani.
Lakini nchi kadhaa tajiri zinazomiliki makampuni makubwa ya dawa zimepinga hatua hiyo, ambayo inaamini kuwa hiyo itakatisha ubunifu
Shirika la Biashara Ulimwenguni, hata hivyo, lilitangaza mwezi uliopita kwamba makubaliano kati ya mataifa tajiri na nchi zinazoendelea kuhusu kuondolewa kwa IP yanaweza kufanyika katika wiki chache tu zijazo.