Muungano wa Kenya Kwanza unapanga kufutilia mbali Hazina ya Kitaifa ya Hifadhi ya Jamii (NSSF) na badala yake kuweka hazina ya jumla ya malipo ya uzeeni, athari za kazi na bima ya ukosefu wa ajira.
Wanawake pia watafurahia haki sawa kama wanaume wakati wa ununuzi na urithi wa ardhi, angalau asilimia 50 ya Baraza la Mawaziri litaundwa na wanawake, wakati nyadhifa za kuteuliwa katika sekta ya umma zitazingatia sheria ya kijinsia ya thuluthi mbili.
Ahadi hizo ni sehemu ya manifesto ya muungano unaoongozwa na Naibu Rais William Ruto iliyozinduliwa jana jijini Nairobi.
Kulingana na manifesto hiyo mfumo wa ‘fit for purpose’ wa hifadhi ya jamii kwa wote utaanzishwa kwani mfumo wa kukatwa kwa mishahara ya NSSF umeshindikana.
Kuhusu wanawake, Kenya Kwanza inajitolea kuweka hatua za kiutawala ili kuhakikisha utekelezaji wa asilimia 100 wa masharti ya kisheria ya ridhaa ya mume na mke katika shughuli za ardhi ili kuwaepusha wanawake na watoto kutokana na kunyang’anywa ardhi ya familia.
Zaidi ya hayo, manifesto inaahidi kutoa msaada wa kifedha na kujenga uwezo kwa wanawake kupitia mfuko wa ‘Hustler’ kwa vyama vya ushirika vinavyoongozwa na wanawake, vyama vya kina mama pamoja na kuanzisha mfuko wa ustawi wa jamii kwa Wanawake wa Kenya wanaofanya kazi nje.
Manifesto inapendekeza kutoa sodo za bure katika shule zote na pia katika vyoo vya umma.
Kwa wazee walio katika mazingira magumu, Kenya Kwanza inajitolea kufikia asilimia 100 ya bima ya afya ndani ya miaka mitatu, kurekebisha programu za uhawilishaji fedha kwa wazee na kaya zilizo katika mazingira magumu ili kuboresha ufanisi na kuharakisha uwajibikaji wa malipo na bima.
Hii ni pamoja na kuwekeza katika elimu na mafunzo kwa walezi na wahudumu wa afya ili kuziba pengo la ujuzi katika utoaji wa huduma maalumu kwa wazee.
Muungano huo unaahidi kujumuisha wanafunzi wote kwenye shule ili kuruhusu watoto wenye ulemavu kuanza kutangamana na umma katika umri mdogo ili kurejesha imani na kujistahi.
Hii ni pamoja na kuongeza usaidizi kwa wanafunzi wenye ulemavu kwa asilimia 50 na kutenga asilimia 15 ya fedha zote za elimu zilizotengwa kwa ajili ya wanafunzi wenye ulemavu na pia kuhakikisha asilimia 100 ya Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya kwa watu wenye ulemavu inawafikia watu wenye ulemavu ndani ya miezi 18.
Zaidi ya hayo, kaunti zitahimizwa kuondoa ada za leseni za biashara mpya zilizoanzishwa na watu wenye ulemavu, huku zikiondoa ushuru wa vifaa vyote vya usaidizi kwa walemavu vinavyoagizwa kutoka nje.
Kenya Kwanza pia imejitolea kutokomeza utapiamlo ndani ya miaka mitano kwa watoto, pamoja na kuboresha matokeo ya kujifunza kwa kuahidi kuunganisha shule zote kwenye mtandao, na kuongeza uwekezaji katika mafunzo mapya ya walimu.