Walinzi wa misitu na watu waliojitolea walipambana na moto na upepo mkali siku ya Jumapili ili kuzima moto mkali unaoendelea katika mbuga ya kitaifa ya Aberdare nchini Kenya kwa takriban saa 24.
Moto huo ulizuka Jumamosi usiku, kulingana na afisa anayefanya kazi katika Shirika la Huduma kwa Wanyamapori nchini (KWS), shirika la serikali linalosimamia mbuga za wanyama, ambaye alisema moto huo “unaenea kwa kasi sana.”
”Moto huo unachoma nyasi, na unasambazwa na upepo mkali,”afisa huyo aliiambia AFP kwa sharti la kutotajwa jina, akieleza kuwa hakuwa na idhini ya kuzungumza na vyombo vya habari.
“Tumehamasisha jamii na wafanyikazi walio karibu kuja pamoja kuzima moto huo na wamejaribu sana wawezavyo … ni kwamba walizidiwa.”
Jina la mbuga hiyo lilinakiliwa katika historia wakati Elizabeth wa Pili wa Uingereza, ambaye wakati huo alikuwa binti wa kifalme alipopokea habari za kifo cha babake alipokuwa akiishi katika hoteli ya Treetops, nyumba ya kulala wageni iliyojengwa juu ya mti katika msitu wa Aberdares.
Rhino Ark, shirika la hisani la uhifadhi nchini Kenya, lilisema kwenye Twitter kwamba limetuma helikopta kufanya uchunguzi wa anga katika eneo hilo ili kukadiria kiwango cha uharibifu katika msitu huo.
The Mount Kenya Trust, shirika lililoundwa kuhifadhi misitu nchini, lilisema Jumapili kwamba timu ya zima moto imeelekea kusaidia kuzima mioto ya misitu huko Aberdares.
Mbuga hiyo iko umbali wa kilomita 100 kaskazini mwa jiji kuu la Nairobi.
Mbuga hiyo ipo katika safu ya milima ya Aberdare, kuna maporomoko ya maji ya kuvutia na misitu mirefu ya mianzi pamoja na aina mbalimbali za wanyamapori wakiwemo chui, tembo na vifaru weusi walio hatarini kutoweka.
Milima ya Aberdares ni safu ya tatu kwa urefu nchini Kenya, ikifikia kilele cha zaidi ya mita 4.000 (futi 13,123).
Katika siku za hivi majuzi, wasiwasi umeongezeka kuhusu pendekezo tata lililowasilishwa bungeni ambalo linaweza kuruhusu wanasiasa kubaini kama msitu wa umma unaweza kuchongwa na kukabidhiwa kwa maslahi ya kibinafsi.
Marekebisho ya Sheria ya Uhifadhi na Usimamizi wa Misitu — mageuzi yaliyopitishwa baada ya miongo kadhaa ya kukithiri kwa ukataji miti — yameibua hasira kubwa kati ya jamii na kuzua hofu kwamba inaweza kusababisha ukataji miti usiodhibitiwa na uharibifu wa mazingira.