Takriban wahamiaji 44 walikufa maji siku ya Jumapili wakati mashua yao ilipopinduka katika pwani ya Sahara Magharibi, shirika la misaada ya wahamiaji Caminando Fronteras lilisema.
Wengine 12 walinusurika kwenye mkasa huo, ambao ulitokea wakati boti hiyo ilipozama kwenye ufuo wa Cap Boujdour, Helena Maleno wa shirika hilo alitweet.
Walionusurika walikamatwa, Maleno aliandika.
Miili ya waathiriwa saba ilirudishwa ufukweni lakini wengine hawakuweza kupatikana, aliongeza.
Hakukuwa na uthibitisho wa mara moja kutoka kwa mamlaka nchini Morocco, ambayo inaona Sahara Magharibi inayozozaniwa kama sehemu muhimu ya ufalme wa Afrika Kaskazini.
Haikuwa wazi mashua hiyo ilikuwa inaelekea wapi, lakini kwa kawaida wahamiaji wanaoondoka kutoka eneo hilo hujaribu kufika Visiwa vya Canary nchini Uhispania.
Morocco ni kitovu muhimu cha kupita kwenye njia zinazochukuliwa na wahamiaji wanaotarajia maisha bora barani Ulaya.
Siku ya Ijumaa, Morocco na Uhispania zilisema katika taarifa ya pamoja zimejitolea kuimarisha ushirikiano katika uhamiaji usio wa halali.
Zaidi ya majaribio 14,700 ya kuhama kinyume na utaratibu yalizuiwa na mitandao 52 ya magendo ya binadamu ilisambaratishwa nchini Morocco katika kipindi cha miezi mitatu ya kwanza ya mwaka huu, kulingana na takwimu za wizara ya mambo ya ndani.
Mamlaka ya Morocco ilisimamisha zaidi ya vivuko 63,120 mwaka jana na kufunga mitandao 256 ya magendo.
Kulingana na wizara ya mambo ya ndani ya Uhispania, zaidi ya wahamiaji 40,000 waliwasili nchini kwa njia ya bahari mwaka 2021. Mwaka huo huo, kulingana na Caminando Fronteras, wahamiaji 4,404 walikufa au kutoweka walipokuwa wakijaribu kufika Uhispania.