Zoezi La Kuhesabu Kura Katika Uchaguzi Mkuu Nigeria Laendelea

(Picha Hisani-Samuel Aranda/The New York Times)

Uchaguzi mkuu nchini Nigeria umeingia siku yake ya nne, huku Tume ya Uchaguzi nchini humo ikizidi kuhesabu kura na kutangaza matokeo kutoka majimboni.

Hata hivyo vyama vikuu vitatu vimelalama kuhusu zoezi hili kuhitilafiwa huku ripoti za kukandamizwa na kuvunja sheria zikitokea ila kwa asilimia ndogo ikilinganishwa na uchaguzi wa hapo awali.

Wagombea 18 wanawania kiti cha Urais kumrithi rais anayeondoka Muhammadu Buhari, ila watatu pekee ndio wameonekana kuwa mibabe. Watatu hawa ni Bola Tinubu kutoka chama tawala cha All Progressives Congress (APC), Atiku Abubakar wa chama cha upinzani cha People’s Democratic (PDP) na Peter Obi wa chama cha Labour Party (LP).


Mwaniaji wa nne Rabiu Kwankwaso anayewania urais kwa tiketi ya chama cha New Nigeria People’s Party (NNPP) anatarajiwa kufanya vyema katika maeneo ya Kaskazini mwa Nigeria .


Kufikia sasa, kulingana na matokeo ambayo yameendelea kutangazwa na Tume ya Uchaguzi nchini Nigeria katika majimbo 36, Tinubu anaongoza akiwa na asilimia 36 ambazo ni kura milioni 7, anafuatiwa na Atiku kwa ukaribu na asilimia 30 ambazo ni kura 6 huku Obi kufikia sasa akiwa amezoa asilimia 20 amabazo ni kura milioni 3.8 ambazo zimehesabiwa.


Waangalizi wa uchaguzi huu mkuu wakiongozwa na Rais mstaafu wa Kenya Uhuru Kenyatta amedokeza kuwa jumla ya wapiga kura milioni 93.4 walipata haki ya kuwachagua viongozi wanaowaenzi.


“Licha ya hali ya usalama kua tishio kubwa, uchaguzi mkuu wa Nigeria umeandaliwa kwa kuzingatia sheria. Umoja wa Afrika umepata ripoti kuhusu maafisa wa tume ya uchaguzi kushambuliwa kabla ya uchaguzi,” alisema Uhuru Kenyatta.


Rais huyo wa zamani ambaye anaongoza Umoja wa Afrika katika uchaguzi huo amewataka raia wa Nigeria kuwa na utulivu wanaposubiri matokeo ya urais.


“Wakati kila mmoja anasubiri tume ya uchaguzi kutangaza matokeo ya urais naomba raia na washikadau wengine kudumisha amani na kusalia wima. Tunawaomba wale ambao hawataridhika matokeo ya uchaguzi huu kutumia njia mwafaka za kisheria kutafta haki,” alisema Uhuru Kenyatta.


Jumla ya vituo vya kupigia kura 176,000 katika majimbo 36 nchini Nigeria vilitumika Jumamosi kwa wapiga kura.