Taasisi ya Kuzuia na kupambana na Rushwa Takukuru Mkoani Mbeya imewafikisha mahakamani watu 14 wakiwemo watumishi wa Halmashauri mbalimbali mkoani humo wakituhumiwa kwa makosa 16 ikiwemo kuendesha genge la uhalifu na utakatishaji wa fedha zaidi ya shilingi Million 350.
Akisoma shtaka hilo la Uhujumu uchumi namba 03/2023 Mwendesha mashtaka wa Serikali kutoka Taasisi ya Kupambana na Rushwa Takukuru Emmanuel Jilugu amewataja washtakiwa kuwa ni Robert Andrew Mpeleta (37) Mfanyabiashara na mkazi wa Iwambi, Anord Jifike Nzali (28) Mfanyabiashara na mkazi wa Dar Es Salaam, Isaya Andembwisye Gerald (27) Mwalimu, Bwigane Seth Mwamelo Afisa mtendaji wa kijiji na mkusanyaji ushuru huko Busokelo, Petr Joseph Mangala ,Wema Joseph Mangala (44) mkazi wa Mapogoro Mbarali na mkusanyaji ushuru, Benedict Salvatory Milinga (40) mkazi wa Block T na mtaalam wa IT na mkusanyaji ushuru, Zueli Abass Mkwama (41) mkazi wa Mbuyuni Mbarali mkusanyaji ushuru.
Amewataja wengine kuwa ni Khalid Abdallah Habibu (30) wa Chimala mkusanyaji wa ushuru, Fashili Fred Lwesya (38) mkulima na mkazi wa Uyole, Shukuru Simbeye (30) mkusanyaji ushuru huko Isongole Ileje, Daniel Juma Mtweve(26) wa Mpemba Tunduma na mkusanyaji ushuru, Ezekia Adamu Mwaisunga (42) mkazi wa Itezi Uyole mkusanya ushuru, Taliki Paulo Samson (25) wa Isenje wilayani Rungwe mkusanyaji ushuru na Ulimboka Adamson Kapyaghile (26) mkusanyaji wa ushuru huko Kata ya Majengo Tunduma.
Wakaili Jilugu amesema washtakiwa wanakabiliwa na mashtaka mbalimbali ikiwemo kosa la kwanza ambalo ni kwa washtakiwa wote 14 nalo ni kuendesha genge la uhalifu kinyume cha aya ya 4 (1) a jedwali la kwanza na sehemu ya 57 (1) na 60 (2) cha sheria ya uhujumu uchumi sura ya 200 iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2022.
Kosa lingine kwa mshtakiwa wa kwanza ni utakatishaji kinyume na kifungu namba 12 (b) na 13 (1) a cha sheria ya utakatoshaji fedha sura ya 423 na marejeo yake 2022 kikisomwa pamoja na aya ya 22 jedwali la kwanza na kifungu namba 57 (1) na 60 (2) ya uhujumu uchumi.
Pamoja na hayo makosa mengine yametajwa kwa washtakiwa wengine wakidaiwa kukutwa wakimiliki mashine haramu za kukusanyia ushuru zijulikanazo kama POS katika maeneo mbalimbali ya mkoa wa Mbeya na Songwe ambapo watuhumiwa wanadaiwa kuwa walilenga kujipatia mamilion ya fedha akiwemo mshtakiwa namba nane ambaye ameelezwa kuwa lengo la kumiliki mashine hiyo ilikuwa ni kumpatia fedha zaidi ya shilingi million miamoja.
Hata hivyo washtakiwa hawakutakiwa kujibu chochote kutokana na mahakama ngazi ya mkoa kutokuwa na mamlaka kisheria kusikiliza shauri hilo.
Kesi hiyo ililazimika kuahirishwa kwa nusu saa kwa ajili ya kupitia vifungu vya dhamana vya sheria ya dhamana ambapo hata hivyo mahakama haina mamlaka ya kufanya hivyo, kwa maana hiyo Hakimu Mkazi katika mahakama ya Hakimu mkazi Mbeya Sangiwa Mtengeti ameahirisha shauri hilo hadi Septemba 11, 2023.
Mawakili wanaowawakilisha washtakiwa kadhaa ni Wakili Sambwee Shitambala, Dr. Tasco Luambano na Kamru Habibu wanaowatetea mshtakiwa wa 1, 2, 3, 9, 10, 12 na 14 huku mawakili wengine wa kujitegemea Gladnes Luhwago na Geofrey Mwakatundu kwa ajili ya mshtakiwa wa 5,7, na 8 na Wakili Febby Cheyo kwa ajili ya mshtakiwa wa sita lakini washtakiwa wawili hawana mawakili hivyo wanajiwakilisha wenyewe.