Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ameagiza kuanzia sasa fomu za kujiunga na shule za serikali sharti zipitiwe na makatibu Tawala wa Mikoa na kuhakikisha zinaeleza wazi kuwa hakuna michango.
Waziri Mkuu ametoa maagizo hayo leo Alhamisi tarehe 30 Juni, 2022, bungeni jijini Dodoma wakati akisoma hotuba yake kuhitimisha Mkutano wa saba wa bunge la 12 ulioanza tarehe 5 Aprili, 2022.
Majaliwa amesema pamoja na mpango wa elimu bila malipo wabunge wamelalamikia kuwepo kwa utitiri wa michango shuleni.
Amefafanua kuwa Serikali kupitia waraka wa elimu namba 6 wa mwaka 2015 imetoa maelekezo bayana kuhusu utekelezaji wa elimu msingi bila malipo ikiwemo matumizi ya fedha za utawala ambazo utolewa na hazina na kupelekwa moja kwa moja katika akaunti za shule husika za msingi na sekondari.
Amesema fedha hizo ni kwaajili ya vifaa vya kufundishia na kujifunzia, ukarabati, uendeshaji wa mitihani ya ndani na utawala.
Pia amesema asilimia 10 ya fedha hizo hutumika kugharamia huduma za umeme, maji na ulinzi.
“Hivyo basi ninaagiza Tamisemi kwa kushirikiana na Sekretarieti za mikoa na Halmashauri zote nchini kufuatilia upatikanaji na taarifa za matumizi ya fedha hizo pamoja na kuhakikisha hakuna michango holela inayotozwa kwa wanafunzi,” amesema Majaliwa na kuongeza;
“Kuanzia sasa hakikisheni maelezo ya kujiunga na shule ya umma yanahakikiwa na kupewa idhini ya Katibu Tawala wa Mkoa husika kwa kushirikiana na maafisa elimu wa wilaya ikiwa inatamka kuwa hakuna michango yeyote holela.”