Jeshi la polisi linamshikilia mtu mmoja, fundi ujenzi na mkazi wa Mlole, Manispaa ya Kigoma Ujiji, Peter Moris (33), Mnyiha kwa tuhuma za kuhusika na mauaji ya watu saba wa familia moja katika Kijiji cha Kiganza, kwa kinachodaiwa wivu wa mapenzi.
Akitoa taarifa hiyo leo, Julai 6, 2022, Kamishna wa Operesheni na Mafunzo ya Jeshi la Polisi nchini, Liberatus Sabas amesema jeshi hilo limejiridhisha bila kuona shaka kuwa mtu huyo ndiye amefanya mauaji peke yake.
Amesema mtuhumiwa huyo alikuwa akimtuhumu mmoja wa marehemu Januari Mussa (35), kwamba alikuwa na mahusiano ya kimapenzi na mkewe.
“Hatua za awali za upelelezi wa awali unaonyesha kiini cha mauaji hayo ni wivu wa mapenzi ambapo mtuhumiwa alikuwa akimtuhumu mmoja wa marehemu kuwa anatembea na mke wake,”amesema Sabas.
Amesema katika tukio hilo kifaa kilichopatikana katika kutekeleza mauaji hayo ni aina ya panga na kwamba mtuhumiwa amekamatwa na mara baada ya upelelezi kukamilika mtuhumiwa huyo atafikishwa mahakamani.
Julai 3, mwaka huu, katika Kijiji cha Kiganza, Wilaya ya Kigoma, mkoani Kigoma, watu sita waliuawa kwa kukatwakatwa na panga sehemu mbalimbali za miili yao huku watoto wawili wakinusurika katika mauaji hayo.
Kati ya watoto hao wawili mmoja James January (4), ambaye alikuwa amejeruhiwa vibaya maeneo ya mgongoni ambapo Julai 5, 2022 alifariki dunia mkoani Morogoro akiwa njiani kuelekea Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kwa ajili ya matibabu zaidi.