Mahakama ya Tanzania kupitia Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki kinachoshughulikia masuala ya kifamilia, ndoa na talaka kilichopo Temeke Dar es Salaam, ina mpango wa kuendesha mashauri saa 24 kutokana na kuzidiwa na wateja.
Kituo hicho ni cha kipekee Afrika na cha pili ulimwenguni, baada ya Singapore, vituo ambavyo vinashughulikia mashauri ya kifamilia ikiwemo talaka na ndoa pamoja na mirathi.
Hayo yamesemwa leo na Mkuu wa Kitengo cha Maboresho ya Mahakama, Dk. Angelo Rumisha wakati Benki ya Dunia ilipotembelea banda la mahakama katika maonesho ya 46 ya Sabasaba, Dar es Salaam.
Amesema baada ya kuwepo kwa kituo hicho kimepokea kesi nyingi, hivyo namna ya uendeshaji wa mashauri hayo umekuwa na changamoto mbalimbali.
“Tumepata changamoto ya watu wengi kutaka huduma kiasi kwamba kuwahudumia imekuwa changamoto, hivyo tunafikiria kufanya kazi saa 24.
“Ili mtu mwenye shauri lake na ni mfanyakazi aende kazini halafu saa 11 au 12 jioni aje mahakamani mpaka saa 2 usiku shauri lake litakaposikilizwa na asubuhi aendelee na majukumu yake kama kawaida, haya ndio maboresho tunayoyazungumzia,” amesema Dk Rumisha.
Amesema mahakama hiyo kwa kushirikiana na Benki ya Dunia wamekuwa wakifanya huduma za uboreshaji wa mahakama katika utoaji haki tangu mwaka 2016.
Amesema serikali ilichukua mkopo katika benki hiyo, ili kuboresha huduma za utoaji haki hivyo wamekuwa wakifuatilia namna gani wanavyoboresha huduma zao.
“Miongoni mwa mambo tuliyoshirikiana nayo ni utoaji haki kwa kutumia mahakama inayotembea ambayo inamfuata mwananchi popote alipo na si mwananchi kufuata mahakama.
“Mahakama hii ipo Sabasaba na inaendelea kutoa huduma,” amesema Dk Rumisha.
Ameongeza kuwa baada ya miaka mitano ya ushirikiano wao na kutokana na mafanikio makubwa ambayo mahakama iliyopata katika uboreshaji wa huduma hizo, waliongeza fedha na muda mpaka 2025 huku ikizingatia katika uwekaji wa miundombinu muhimu ya kurahisisha upatikanaji wa haki kwa wote.
Amesema ujenzi wa mahakama ni kitu kidogo katika maboresho hayo, wanachozingatia zaidi ni kupunguza muda wa kesi kukaa mahakamani, kupunguza mrundikano wa mashauri yaliyokaa muda mrefu na namna ya kutoa haki kwa makundi maalum ikiwemo wajane, watoto na wenye mahitaji maalum.
“Hauwezi kupunguza mashauri bila kupunguza gharama za kesi ikiwemo umbali wa kufuata mahakama. Ndio maana tumejenga Mahakama Kuu Lindi ili kumsaidia mwananchi wa Marendego ambaye anatumia kilometa 370 kwenda Mtwara kupata haki, kujenga Mahakama Kuu Singida, Manyara Geita,” amefafanua.
Amesisitiza kuwa ujenzi wa mahakama utasaidia kupunguza gharama za uendeshaji wa kesi ili kuwarahisishia wananchi.