Uamuzi kesi ya kina Mdee na wenzake kutolewa leo.

Mahakama Kuu Masijala Kuu leo inatarajiwa kutoa uamuzi wa ombi la Mbunge wa Viti Maalumu, Halima Mdee na wenzake 18 endapo wapewe kibali cha kufungua kesi kupinga kuvuliwa uanachama wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) au la.

Mdee na wenzake waliwasilisha maombi hayo Mei 13, mwaka huu wakiomba mahakama iwapatie kibali cha kufungua kesi ya mapitio ya kimahakama dhidi ya Baraza la Wadhamini la Chadema, Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG). Juni 30, mwaka huu maombi hayo yalisikilizwa na Jaji Mustapha Ismail na kupanga kutoa uamuzi leo saa 6:00 mchana.

Katika maombi hayo, Mdee na wenzake wamesimamia hoja kuwa, uamuzi uliotolewa na Baraza Kuu la Chadema unagusa maslahi ya wabunge hao, kwamba kuna kesi ya kubishaniwa, kwamba maombi hayo yalifunguliwa kwa wakati na pia Chadema ni chombo cha umma.

Katika hoja husika, Wakili wa wabunge hao, Ipilinga Panya alidai anaona uamuzi huo unagusa maslahi ya wabunge hao kwa kuwa unagusa moja kwa moja hali ya ubunge wao kwa kuwa kwa kuvuliwa uanachama wanapoteza sifa ya kuwa wabunge.

Kuhusu hoja ya muda, Panya alidai maombi hayo yalifunguliwa Mei 13, mwaka huu siku moja baada ya uamuzi wa Baraza Kuu la Chadema kuwafukuza uanachama, hivyo yalikuwa ndani ya muda uliowekwa kisheria na wana haki ya kusikilizwa na mahakama.

Kuhusu kuwapo kesi ya kubishaniwa, Wakili Aliko Mwamanenge alidai wanaona ipo kesi ya kubishaniwa kwa kuwa katika maombi hayo wapeleka maombi wote kupitia viapo vyao walidai hawakupewa muda wa kusikilizwa wakati wa uamuzi uliotolewa na Kamati Kuu ya Chadema Novemba 27, 2021 hata ule wa Baraza Kuu wa Mei 11, 2022.

Lakini pia alidai katika viapo vyote imeonekana kuna msukumo kutoka kwa mjibu maombi wa kwanza kumshinikiza Spika wa Bunge achukue hatua dhidi ya wabunge hao baada ya uamuzi wa Baraza la Chadema. Kuhusu hoja kuwa Chadema ni chombo cha umma au binafsi, Wakili Edson Kilatu alidai kwamba kwa uamuzi wa baraza hilo, lilikuwa likifanya kazi ya umma.