Aliyetumika kufanya mauaji kwakukodiwa nchini Tanzania naye auawa.

Mkazi wa Kijiji cha Kapanga wilayani Tanganyika, Heleni Nyankole maarufu Beberu (36), anayedaiwa kuwa kinara wa kufanya mauaji ya kukodiwa, ameuawa kwa kupigwa risasi.

Kamanda Polisi Mkoani Katavi, ACP Ally Makame amesema mtuhumiwa huyo aliuawa usiku wa kuamkia jana wakati wa akipambana na polisi.

Kamanda Makame amesema kuwa Beberu anadaiwa kukodiwa kufanya mauaji ndani ya Mkoa wa Katavi na nje ya mkoa huo.

Amesema June 28, 2022 usiku katika kijiji Bukombe mtuhumiwa huyo anadaiwa kumuua mkazi wa Kijiji cha Bukombe Tanganyika, Mandalu Ndulu (36) kwa kumkata na kitu chenye ncha kali shingoni.

Kamanda Makame amesema kuwa Beberu alikodiwa na watu wawili wakazi wa kijiji cha Luhita-Bujombe kwa makubaliano ya kumlipa shilingi 800,000 ili amuue Ndulu.

Amesema polisi baada ya kupata taarifa za tukio hilo waliwakamata watuhumiwa hao wawili baada ya kuwahoji walikiri kumkodi mtuhumiwa huyo ambapo walimpa shilingi 300,000 ikiwa ni malipo ya awali kisha kutekeleza mauaji hayo.

“Tulianza msako mkali Julai 7,2022 usiku tulimkamata  mtuhumiwa huyo wa mauaji kijiji cha Lwega wilayani Tanganyika akiwa amelala ndani ya nyumba yake, polisi walipomuamuru kujisalimisha alikaidi,”

“Alipanda juu ya dari kisha kutoboa paa la nyumba iliyoezekwa kwa nyasi kwa kutumia panga, akiwa juu alijaribu kushuka, ghafla alishuka akiwa na kipande cha nondo kwa lengo la kumjeruhi askari,” amasema

Kamanda Makame amesema kuwa askari walifyatua risasi hewani ili kumuonya lakini alikaidi na kuendelea kuwafuata.

“Walifyatua nyingine ikamjeruhi tumboni, alipoteza maisha wakati anakimbizwa kituo cha afya” ameeleza.

Inadaiwa kuwa mtuhumiwa huyo alikuwa anatafutwa na polisi kwa muda mrefu kwa tuhuma za kukata mapanga watu maeneo tofauti.