Rais wa Ufilipino, Ferdinand Marcos Jr amesema nchi hiyo haina mpango wa kujiunga tena na Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu, huku mwendesha mashtaka wa mahakama hiyo akitaka kuanzisha upya uchunguzi kuhusu vita vya mauaji ya rais wa zamani Rodrigo Duterte.
“Ufilipino haina nia ya kujiunga tena na ICC,” Marcos Jr aliwaambia waandishi wa habari, baada ya hapo awali kuonyesha kwamba hatashirikiana na uchunguzi huo.
Duterte aliiondoa Ufilipino kutoka mahakama ya ICC mwaka 2019 baada ya kuanzisha uchunguzi wa awali kuhusu ukandamizaji wake wa dawa za kulevya, ambao uliua maelfu ya watu.
Majaji wa ICC waliidhinisha uchunguzi kamili kuhusu kampeni ya kupambana na dawa za kulevya Septemba mwaka jana, wakisema inafanana na shambulio lisilo halali na la kimfumo dhidi ya raia.
ICC ilisimamisha uchunguzi huo miezi miwili baadaye, baada ya Manila kusema ilikuwa inachunguza madai ya uhalifu yenyewe.
Lakini mwendesha mashtaka wa ICC, Karim Khan alisema mwezi Juni kwamba ombi la Manila la kuahirisha uchunguzi huo halikukubalika na kwamba unapaswa kuanza upya “haraka iwezekanavyo”.
Marcos Mdogo, ambaye aliunga mkono vita vya dawa za kulevya, alichaguliwa kuwa rais kwa kishindo mwezi Mei kwa usaidizi wa ushirikiano na bintiye Duterte, Sara, ambaye alishinda kinyang’anyiro cha makamu wa rais.