Hakuna homa ya Nyani Tanzania

Mganga Mkuu wa serikali nchini Tanzania, Dkt. Aifello Sichalwe amesema, mpaka sasa nchini humo hakuna mgonjwa aliyethibitika kuugua homa ya Nyani 

Dkt. Sichalwe amesema kumekuwa na maswali mengi yanayoonesha baadhi ya wananchi wana hofu kuhusu homa hiyo ya nyani, lakini serikali inafuatilia kwa taarifa za kila mgeni anayeingia nchini ambapo hadi sasa hakuna mgonjwa wa homa hiyo.

Dkt. Sichalwe amewataka Watanzania kuchukua tahadhari za ugonjwa huo na kutoa taarifa kwa mamlaka husika pale wanapoona dalili za ugonjwa wasioufahamu ili serikali ichukue hatua za haraka kudhibiti.

Homa ya Nyani husababishwa na wanyama aina ya Nyani na Panya, ambapo mgonjwa huwa na muonekano wa malengelenge hasa maeneo ya mikono yanayofanana na ugonjwa wa Tetekuanga.

Julai 23 WHO ilitangaza kuwa homa ya nyani ni dharura ya afya ya umma duniani, hatua ambayo inalenga kuwezesha shirika hilo kuratibu na kushirikiana na nchi na wadau halikadhalika mshikamano wa kidunia.