Mkazi wa Mkolani mkoani Mwanza Shabani Budeba (60), amehukumiwa kifungo cha maisha jela na Mahakama ya Wilaya ya Nyamagana baada ya kumtia hatiani kwa kosa la kumnajisi mtoto wake wa kambo mwenye umri wa miaka 12 anayesoma darasa la nne.
Kesi namba 33 ya mwaka 2022 dhidi ya Budeba ilisikilizwa na Hakimu wa Mahakama hiyo, Juma Mpuya.
Budeba alihukumiwa kifungo hicho katika mahakama hiyo baada ya kusikilizwa ushahidi ukiwamo wa mtoto, mama mzazi, majirani na daktari aliyempima mtoto huyo.
Mahakama hiyo ilielezwa kuwa mshtakiwa huyo alitenda kosa hilo kwa nyakati tofauti akiwa nyumbani kwake mwezi Januari hadi Februari mwaka huu baada ya mtoto huyo kutoka nyumbani kwa mama yake eneo la Buhongwa na kwenda nyumbani kwa baba yake wa kambo.
Upande wa mashtaka uliongozwa na Wakili wa Serikali, Gati Mathayo, na Mwendesha Mashtaka, Lupyana Mahenge uliwasilisha mashahidi sita akiwamo mtoto aliyenajisiwa.
Shahidi wa kwanza, mtoto, alidai kuwa akiwa nyumbani kwa mshtakiwa huyo, alimwambia alale kwenye nyumba ndogo tofauti na nyumba waliyokuwa wamelala watoto wengine wa familia hiyo ndipo usiku alipoingia ndani na kufunga mlango kisha kuanza kumnajisi.
Alidai alitishiwa na mshtakiwa kwamba angeuawa kama angetoa taarifa hizo, hivyo kusababisha mtoto huyo kuendelea kukaa kimya akihofia kuuawa.
Shahidi wa pili, mama mzazi wa mtoto huyo, alidai kuwa siku moja alipokwenda nyumbani kwa mwanaume huyo kumfuata binti yake, alipewa taarifa na mmoja wa majirani kwamba mtoto wake amekuwa akinajisiwa na alipomuuliza alikiri kufanyiwa kitendo hicho.
Mama huyo alidai kuwa baada ya kupata maelezo ya mtoto wake, alitoa taarifa polisi kisha taratibu zingine za kesi kuanza ikiwamo mtoto kupelekwa hospitalini kufanyiwa vipimo vilivyobaini alitendewa kitendo hicho.
Akijitetea mbele ya mahakama hiyo, Budeba alidai hahusiki na tukio hilo na kumtaka mtoto huyo aseme lini alikwenda nyumbani kwake akatendewa kitendo hicho.
Alijitetea kuwa vipimo vya mtoto huyo vilichukuliwa na daktari bila kuwapo mpelelezi.
Hakimu Mpuya akisoma hukumu ya kesi hiyo, alisema mahakama hiyo imeridhishwa na ushahidi uliotolewa na upande wa Jamhuri na mtoto huyo, umejitosheleza pasipo kuacha shaka.
Alisema tangu afikishwe mahakamani huko kwa kosa hilo hakuna ndugu, majirani wala mke wake waliokwenda kumwona wala kumtolea dhamana, jambo ambalo linaonyesha alitenda kosa hilo.
Kabla ya hukumu hiyo, mshtakiwa alipewa nafasi ya kujitetea na aliomba mahakama impunguzie adhabu kwa kuwa anategemewa na wazazi wake na watoto wake watano.
Hata hivyo, Hakimu Mpuya alikataa kumpunguzia adhabu hiyo kwa kuwa kipindi anatenda kosa hilo alikuwa anafahamu kuwa kuna watu wanamtegemea.
“Mtoto wa kambo ni mtoto wako, ulipaswa kumlinda, umetenda kitendo cha kinyama zaidi ya mbuzi na ng’ombe, hivyo ninakuhukumu kifungo cha maisha ili iwe fundisho kwako na kwa watu wengine wanaojihusisha na vitendo vya namna hiyo,” Hakimu Mpuya alihitimisha.