Notice: Function _load_textdomain_just_in_time was called incorrectly. Translation loading for the wordpress-seo domain was triggered too early. This is usually an indicator for some code in the plugin or theme running too early. Translations should be loaded at the init action or later. Please see Debugging in WordPress for more information. (This message was added in version 6.7.0.) in /home/mwanzotv/public_html/wp-includes/functions.php on line 6114
Masauni ataka uchunguzi kuhusu maiti zilizookotwa kwenye viroba - Mwanzo TV

Masauni ataka uchunguzi kuhusu maiti zilizookotwa kwenye viroba

Waziri wa Mambo ya Ndani nchini Tanzania, Hamadi Masauni ameliagiza Jeshi la Polisi nchini humo kuhakikisha linafanya uchunguzi wa kina ili kubaini waliohusika na mauaji ya watu wawili na kuwatupa wakiwa kwenye viroba.

Maiti hizo ziliokotwa Agosti 11, 2022 zikiwa kwenye viroba katika kata ya Tunguli wilayani Kilindi mkoani Tanga na kupelekwa kuhifadhiwa katika Hospitali Teule ya Wilayani Kilindi.

Masauni ametoa agizo hilo jana Jumatano Agosti 17, 2022 baada ya kufika katika chumba cha kuhifadhia maiti cha Hospitali Teule ya Wilayani Kilindi mkoani Tanga ilipohifadhiwa miili hiyo.

Waziri huyo amesema amesikitishwa na tukio hilo la mauaji lililotokea Wilayani humo na kuagiza Jeshi hilo lishirikiane na vyombo vingine vya usalama kuendeleza uchunguzi ili kuwakamata waliofanya mauaji hayo.

“Tukio hili ni la kinyama dhidi ya raia wenzetu wa Kitanzania, jambo hili halikubaliki kwa namna yoyote ile na sio utamaduni wetu. Kama Serikali tumelichukulia kwa uzito unaostahili na tutafanya kila linalowezekana ili vyombo vyetu vya usalama vinawabaini na kuwakamata wahusika,” amesema Waziri huyo.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Omari Mgumba amesema watu waliofanya tukio hilo linaonyesha ni wazoefu sababu namna walivyo wakunja kwenye kiroba cha kilo 50 lakini utazani nikilo 20.

Mgumba amesema kuwa dalili za awali zinaonyesha kuwa mauaji hayo hayajafanyika mkoa wa Tanga bali sehemu nyingine na kupeleka kutupa katika eneo hilo.

Kwa upande wake, Kamanda wa Polisi Mkoani Tanga, Sofia Jongo amesema tayari Jeshi la Polisi nchini limeshaunda kamati kwaajili ya uchunguzi wa tukio hilo.

Kwa upande wake Mbunge wa Kilindi (CCM) Omari Kigua amesema tukio hilo linaweza kuwakimbiza wawekezaji wanaotaka kuwekeza huku akiliomba Jeshi la Polisi kuendelea na uchunguzi ili kuwabaini waliotekeleza tukio hilo la kinyama.