Mahakama ya Wilaya ya Babati Mkoani Manyara, imemhukumu kutumikia kifungo cha maisha jela mkazi wa Kijiji cha Imbilili, Juma Gidera (40) kwa kosa la kumlawiti mjukuu wake wa kiume wa miezi sita.
Hukumu hiyo imetolewa na hakimu mkazi mfawidhi wa mahakama ya wilaya ya Babati Victor Kimario baada ya kusikiliza pande zote mbili na kujiridhisha pasipo na kutia shaka.
Kimario amesema mahakama imemtia hatiani mshtakiwa huyo baada ya kusikiliza mashahidi sita wa Jamhuri na mshtakiwa hakuwa na shahidi yeyote bali aliamua kukaa kimya.
Awali akisoma hukumu hiyo amesema mshtakiwa huyo ametenda kosa hilo Mei 26 mwaka huu katika Kijiji cha Kiru six kata ya Kiru.
Hakimu huyo amesema mahakama hiyo imejiridhisha pasipo na shaka baada ya kusikiliza shahidi wa kwanza na wa pili ambao ni ndugu wa mshtakiwa waliotoa ushahidi unaothibitisha Gidera kumlawiti mjukuu wake.
Amesema ushahidi mwingine uliomtia hatiani ni ushahidi wa daktari ambao ulithibitisha kuwa alimuingilia mtoto huyo ambaye ni mtoto wa mtoto wake kinyume na maumbile.
Amesema mshtakiwa huyo kosa alilolifanya ni kinyume na sheria ya kanuni ya adhabu kifungu cha 154(1) (a) (2) sura ya 16 iliyofanyiwa marejeo mwaka 2019.
Naye wakili wa serikali Shaban Mwegole ameiomba mahakama hiyo kutoa adhabu kali kwa mshtakiwa inavyosema kuwa mtu anayemuingilia kinyume na maumbile mtoto chini ya miaka 10 afungwe maisha.
Kwa upande wake Juma Gidera alipopewa nafasi ya kujitetea alikaa kimya hivyo ikaonekana ikiwa ni ishara kuwa amekubaliana na ushahidi uliotolewa mahakamani.