Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) umetoa siku 11 kwa waajiri wenye malimbikizo ya madeni ya michango ya watumishi kuhakikisha wanalipa haraka kabla ya Agosti 30 mwaka huu.
Hivi karibuni, NHIF iliingia katika sintofahamu kati yake na baadhi ya wanachama baada ya kushindwa kupata huduma hasa wategemezi (wazazi) kutokana na kutohuisha taarifa pamoja na baadhi ya maboresho ambayo mfuko huo uliyatangaza ikiwamo mwanachama kutobadilisha kituo cha matibabu kwa siku 30.
Taarifa kwa umma iliyotolewa leo Agosti 19, 2022 na Kitengo cha uhusiano NHIF imeeleza kuwa hatua zitachukuliwa kwa waajiri ambao hawatakamilisha michango hiyo.
“Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya unawatangazia waajiri wote nchini wenye malimbikizo ya madeni ya michango ya watumishi wao kulipa haraka malimbikizo hayo kabla ya Agosti 30, 2022 ili kuondoa usumbufu unaoweza kujitokeza kwa wanufaika wao wanapohitaji huduma za matibabu.
“Baada ya muda huo kupita mfuko utalazimika kuchukua hatua stahiki kwa mujibu wa sheria ya mfuko. Ikumbukwe kwamba mfuko uliwakumbusha waajiri wote kupitia tangazo lake Machi mwaka huu ambapo baadhi ya waajiri wameshindwa kulipa malimbikizo husika,” ilieleza taarifa hiyo.