Mwakyembe kuongza jopo la uchunguzi malalamiko ya mitihani ya Uanasheria

Waziri wa Katiba na Sheria, Dk Damas Ndumbaro amemteuwa Dk Harison Mwakyembe kuwa Mwenyekiti wa kamati ya watu saba ili kutafuta chanzo cha kufeli kwa wingi katika mitihani ya mafunzo ya Uanasheria kwa Vitendo (LST).

Wajumbe wengine katika kamati hiyo ni Jaji Mstaafu Cililius Matupa aliyewahi kuwa mshauri wa rais Dk Jakaya Kikwete, Rashid Asaa ambaye ni Mwenyekiti wa Tume ya Maadili ya Viongozi wa Umma wa Zanzibar.

Wengine ni Gloria Kalabamu, Makamu wa Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika, Alice Mtulo, Wakili mwandamizi kutoka Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali, Mary Mniwasa, Kaimu Mtendaji Mkuu wa Dar Stock Exchange na John Kaombwe ambaye ni Mwanafunzi aliyehitimu LST.

Hayo yamebainishwa leo Jumatano Oktoba 12, 2022 na Waziri wa Katiba na Sheria, Dk Damas Ndumbaro alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kuhusu sakata la kufeli katika Taasisi ya Mafunzo ya Uanasheria kwa Vitendo Tanzania (LST).

Kuundwa kwa tume hiyo kumekuja baada ya kelele za wananchi kufuatia hoja iliyoibuliwa na gazeti la mwananchi kuhusu kiwango cha idadi ya waliofeli mtihani wa mwisho kwa elimu ya vitendo katika taasisi hiyo.

Waziri amesema kamati hiyo itakabidhiwa hadidu rejea na Kàtibu Mkuu wa Wizara hiyo, Mary Makondo kesho Oktoba 13, 2022 na itafanya kazi kwa siku 30.

“Baada ya hapo, Mwenyekiti wake atakuja hadharani kutoa taarifa kwa waandishi kuhusu walichobaini lakini muamini kamati ina watu wenye weledi mkubwa sana,” amesema Dk Ndumbaro.

Hata hivyo amesema takwimu za miaka ya nyuma zinaonyesha shule hiyo imekuwa ikifaulisha kwa kiwango cha wastani wa asilimia 81.